Katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amejitosa kwenye mjadala wa viongozi wa dini kuzungumzia siasa, akisema waachwe wazungumze kwa kuwa wameona kasoro za kiutendaji serikalini.
Amesema katika hali ya kawaida viongozi hao hawawezi kukurupuka, kwa hiyo ni lazima kuna tatizo wameliona na kwamba kauli zao hizo zinalenga kujenga Taifa, si kubomoa.
Mjadala huo umeibuka baada ya viongozi wa dini kutumia ibada za sikukuu ya Mwaka Mpya kuikosoa Serikali, baadhi wakisema haiheshimu utawala wa sheria, wananchi kutopewa uhuru wa kutoa maoni yao, viongozi kukubali kukosolewa huku wengine walizungumzia kuhusu haki na amani.
Miongoni mwao ni Askofu Zachary Kakobe aliyeitaka Serikali ibadilishe Katiba na kurudi kwenye mfumo wa chama kimoja kama inaona ndio sahihi kuliko kuvinyima vyama vya upinzani nafasi ya kutekeleza wajibu wao.
Baadaye Mamlaka ya Mapato (TRA) ilitangaza kuwa itachunguza utajiri wake baada ya kusikika akisema kuwa ana fedha kuliko Serikali, huku katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani akiwataka viongozi wa dini kuacha kuzungumzia siasa madhabahuni.
“Hata wakati wa utawala wa (Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya) Kikwete na (wa Awamu ya Pili, Ali Hassan) Mwinyi, viongozi wa dini walikuwa wakitoa maoni yao na kusikilizwa,” alisema Maalim Seif.
Waziri kiongozi huyo wa zamani wa Zanzibar alikuwa akitoa maoni yake baada ya kuombwa na gazeti hili kutoa tathmini yake ya mwaka 2017.
Wamehisi kuna jambo
Alisema viongozi wa dini wamehisi kuna kasoro fulani ndani ya Serikali ndiyo maana wamesema hayo na kwamba, si jambo jipya kutokea kwa kuwa walishawahi kukosoa Serikali zilizopita.
Alisema wakati wa utawala wa Mwinyi na Kikwete, kulikuwa na barua za kichungaji za kuisema na kuikosoa Serikali, lakini marais hao wote walikuwa wavumilivu na walisikiliza maoni yao.
“Yale yanayofurahisha yachukuliwe na yale yanayokera vumilia. Kisha uyachukue na ujiulize hivi ni kweli aliyoyasema baba askofu au ameweka chumvi?” alisema Maalim Seif ambaye amewahi pia kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Alibainisha kuwa kiongozi anatakiwa kusikiliza zaidi kauli za kumkosoa ili azifanyie kazi huku akitahadharisha kwamba kuna watu kazi yao ni kusifia viongozi hata katika jambo lisilo na msingi na kuonya kuwa hao ni hatari zaidi.
“Kauli za kukosoa azifanyie kazi kuliko za kumsifia. Lazima atambue kuwa kuna watu wanajipendekeza kwa kusifia viongozi na kuwapandisha chati hadi mbinguni kwa sababu ya masilahi yao,” alisema.
“Umakini unahitajika hapa, hasa kwa watu wanaopenda kusifusifu kwa kila jambo. Wale wanaokosoa ndiyo wasikilizwe zaidi. Utawala wa Magufuli una mazuri na wanasiasa wasione tabu kuyasema na watawala wasione aibu kukoselewa, bali wavumilie.
“Marehemu (Spika wa Bunge la Tisa, Samuel) Sitta aliwahi kusema mwanasiasa lazima uwe na ngozi ngumu ya kuvumilia.”
Ampongeza Magufuli
Maalim Seif pia alimpongeza Rais Magufuli kwamba amejitahidi kudhibiti utoroshwaji wa madini na kuhakikisha rasilimali hizo zinawanufaisha Watanzania.
“Amepambana na rushwa kwa sasa imepungua. Amerejesha nidhamu serikalini. Kwa sasa si rahisi kukuta rushwa, ingawa bado kuna maeneo ipo. Awamu hii imejitahidi kupambana na mapapa wa rushwa na si vidagaa,” alisema.
Hali ngumu ya maisha
Kuhusu takwimu za uchumi kuonekana kukua huku wananchi wakidai fedha zimepungua mifukoni, alisema: “Mwaka 2017 wananchi wengi walikuwa na matumaini makubwa ya kuwa na maisha mazuri, lakini imekuwa kinyume. Hali ni ngumu. Ugumu wa maisha si Bara tu hata huku Zanzibar.
“Pale Dar es Salaam baadhi ya wafanyabiashara wamefunga maduka yao. Ingawa Serikali kwa nyakati tofauti inasema uchumi unakua, lakini si kweli. Tunataka hali ya uchumi iendane na hali halisi ya maisha ya wananchi. Takwimu za kwenye makaratasi hazitasaidia.”
Agusia demokrasia
Kuhusu demokrasia, Maalim Seif alisema kwa sasa imerudi nyuma hasa baada ya Rais Magufuli kupiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano licha ya kuwa mambo hayo yapo kwa mujibu wa sheria. “Kupiga marufuku mikutano ya hadhara kumeathiri utendaji kazi wa vyama vya siasa. Kazi ya chama cha siasa ni kuwatafuta wanachama ambao hawapatikani kama vyama havielezi sera na mikakati yao. Usipopata nafasi hiyo huwezi kufanikiwa,” alisema.
Chanzo-Mwananchi
Social Plugin