Wakati mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu akiwa amewasili nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi, ubalozi wa Marekani nchini umesema uko tayari kusaidia uchunguzi dhidi ya shambulio lake iwapo utaombwa.
Mbali na ubalozi huo, Umoja wa Ulaya (AU) nao umesema unategemea kuona maendeleo mazuri kutokana na uchunguzi wa tukio hilo unaoendelea.
Familia ya Lissu na chama chake cha Chadema vimekuwa vikisisitiza haja ya uchunguzi wa shambulio dhidi ya Lissu lililofanywa na watu wasiojulikana mjini Dodoma, ufanywe na taasisi huru na mwishoni mwa wiki mwanasheria huyo wa kujitegemea aliomba jumuiya ya kimataifa iingilie kati.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi limekuwa likisema kuwa bado lina uwezo wa kuchunguza tukio hilo.
Pia Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alisema uchunguzi ulikamata magari zaidi ya kumi 10 yanayofanana na lililotajwa kuhusika katika tukio hilo, lakini hakuna mtu aliyekamatwa.
Baadaye Oktoba 8, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro alisema mjadala wa tukio hilo umefungwa.
Kwa sasa Lissu, aliyekuwa akitibiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya ameruhusiwa kutoka na amehamishiwa Ubelgiji kwa matibabu ya awamu ya pili yakayohusisha mazoezi baada ya mifupa yake kuharibiwa na risasi katika shambulio hilo la Septemba 7.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa alisema jana kuwa chombo hicho hakizungumzii suala la Lissu.
Akijibu swali la gazeti lililomtaka kutoa maoni yake kuhusu kutokubaliwa kwa wachunguzi wa kimataifa kusaidia upelelezi dhidi ya shambulizi la Lissu, ofisa ubalozi wa Marekani nchini alisema kwa njia ya barua pepe kuwa itakuwa tayari kutoa ushirikiano wake ikiwa itaombwa na Serikali ya Tanzania.
“Wakati Serikali ya Marekani huko nyuma imekuwa ikitoa ushirikiano katika baadhi ya uchunguzi wa kimataifa, kufikiria uwezekano wa kushiriki, utahitaji kwanza ombi la msaada kutoka Serikali ya Tanzania,” inasema barua pepe kutoka ubalozi wa Marekani.
Barua hiyo pepe inataka mtoaji taarifa hiyo anukuliwe kama ofisa ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam.
Lissu alishambuliwa wakati akiwa nje ya makazi yake mjini Dodoma, akiwa ndani ya gari lake.
Mbunge huyo aliwaambia waandishi wa habari jijini Nairobi kuwa nyumba hiyo ni moja ya zile za viongozi zilizopo eneo hilo ambazo zinalindwa wakati wote na kwamba eneo la kuingilia kwenye nyumba hizo lina geti ambalo hukaa askari wakati wote, lakini siku hiyo hawakuwepo.
Kama Marekani wataombwa kushiriki uchunguzi huo, haitakuwa mara ya kwanza kuja nchini. Mwaka 2013 Shirika la Uchunguzi la Marekani (FBI) lilichunguza mauaji ya aliyekuwa Paroko wa Parokia ya Mpendae, Padri Evarist Mushi aliyeuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Hata hivyo, mtuhumiwa aliyebainishwa na FBI, Mussa Omar Makame alikuja kuachiwa na Jeshi la Polisi baada ya ushahidi kutotosha kumtia hatiani.
Mbali na kauli hiyo ya ubalozi huo, mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Balozi Roeland van de Geer ameliambia gazeti hili kwa njia ya barua pepe kuwa jumuiya hiyo imekuwa ikifanya majadiliano na Serikali kuhusu masuala ya haki za binadamu, siasa na uchumi yanayoibuliwa na kwamba unaamini uchunguzi wa shambulio la Lissu utapiga hatua.
“Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wake wana mazungumzo ya mara kwa mara yakiwemo ya kisiasa yaliyowekewa utaratibu rasmi, masuala yanayohusu haki za binadamu pamoja na siasa na kiuchumi kwa pande zote, Tanzania na Ulaya huibuliwa na kujadiliwa,” inasema baruapepe ya Balozi Geer.
“EU na wanachama wake na Tanzania wataendelea na mazungumzo haya ikiwa ni pamoja na matukio ya kisiasa ya hivi karibuni. EU inaamini kuwa kutakuwa na maendeleo katika uchunguzi wa jaribio la maisha ya Lissu.”
Hata hivyo, Wakili maarufu nchini, Dk Onesmo Kyauke alisema suala la kuita vyombo vya kimataifa kuchunguza ni gumu kwa sababu linaingilia mamlaka ya ndani ya nchi.
“Kila nchi ina vyombo vyake vya usalama vinavyoshughulikia uhalifu wa ndani. Nchi inaweza kuomba msaada wa kimataifa kama kuna makosa yaliyovuka mipaka kama ugaidi au kutakatisha fedha, lakini makosa ya ndani inakuwa vigumu, kwa sababu lazima waseme wameshindwa,” alisema Dk Kyauke.
Alisema bado ana imani ya vyombo vya ndani vya usalama, hata kama vimekaa kimya.
Aliongeza kuwa sheria zinaruhusu watu kufanya uchunguzi wao binafsi, lakini pia zinaruhusu mwendesha mashtaka wa Serikali kuuchukua uchunguzi huo kwa manufaa ya Serikali.
“Zipo sheria zinazoruhusu watu kufanya uchunguzi wao binafsi, lakini pia sheria hizo hizo zinampa mamlaka DPP kuchukua suala hilo kwa manufaa ya Serikali.”
Alipoulizwa maoni yake kuhusu suala hilo, Profesa wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Ruaha mkoani Iringa, Gaudence Mpangala alisema shambulio la Lissu limeshachafua taswira ya Tanzania kimataifa.
“Hili suala lina impact (athari) kubwa kimataifa, siyo la kuchukulia kijuujuu,” alisema.
Profesa Mpangala alipendekeza kuwepo mjadala kujadili demokrasia na uhuru wa maoni.
Alisema ni muhimu kujadili suala hilo kwa kuwa hata wakati wa mfumo wa chama kimoja, muasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alikubali kukosoa Serikali.
Na Elias Msuya, Mwananchi
Social Plugin