Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi 'Sugu' na mratibu wa chama hicho Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga wameitwa Polisi wakisema hawajui sababu ya wito huo.
Hata hivyo, wawili hao wamesema wanahisi wito huo unatokana na mkutano wa hadhara alioitisha Sugu katika viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.
Akizungumza kwa simu leo Jumanne Januari 2,2018 Sugu amesema juzi jioni alipigiwa simu na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya (RCO) kwamba pamoja na Masonga wafike jana ofisini kwake kuzungumza lakini alimueleza ilikuwa ni siku ya sikukuu hivyo itakuwa ngumu kwenda, hivyo walikubaliana wafike leo.
"Walinipigia simu juzi jioni wakinitaka mimi na Masonga twende makao makuu ya polisi jana, nikawaambia itakuwa ni sikukuu hivyo tukakubaliana leo asubuhi, hivyo tupo njiani tunaelekea huko kuitika wito. Sijajua sababu, lakini nadhani ni uchochezi," amesema Sugu.
Masonga amesema anaamini sababu ya kuitwa kwao inatokana na mkutano wao na wananchi.
Amesema katika mkutano huo yeye Masonga ndiye aliyemkaribisha Sugu kuzungumza na wananchi na alifunga mkutano, lakini kabla ya kumkaribisha alizungumza machache kuhusu mustakabali wa Taifa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga hajapatikana ili kuzungumzia wito huo wa akina Sugu.
Social Plugin