BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), inatarajia kuanza kampeni ya kuwasaka jumla ya wanufaika 119,497 nchini, ambao wamekiuka sheria iliyoanzisha bodi hiyo kwa kutoanza kurejesha mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 285, waliyokopeshwa tangu 1994/1995 na mikopo yao imeiva.
Aidha, bodi hiyo inatarajia kuanza kufanya ukaguzi kwa waajiri mbalimbali nchini kote ili kubaini kama katika orodha za waajiriwa wao, kuna wanufaika wa mikopo ambao hawajaanza kurejesha.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru alisema msako huo unaanza Jumatatu Januari 8, 2018 na utafanyika kwa miezi mitatu.
Akitoa tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya bodi hiyo kwa nusu ya mwaka wa fedha wa 2017/2018 uliomalizika Desemba 31 mwaka jana, alisema wana mpango wa kuboresha ufanisi katika utoaji wa mikopo ya elimu ya juu na ukusanyaji wa mikopo iliyoiva.
Alisema maofisa wa bodi, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Serikali, wamejipanga kutekeleza hilo ili kuongeza makusanyo ya mwezi kutoka wastani wa Sh bilioni 13 hivi sasa hadi kufikia Sh bilioni 17 mwezi Juni 2018.
Akifafanua, Badru alisema kuwa kila mwajiri, ana wajibu wa kisheria wa kuwasilisha makato ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kwa bodi ndani ya siku 15 baada ya mwisho wa mwezi, lakini baadhi ya waajiri wamekuwa hawafanyi hivyo na kuilazimisha Bodi ya Mikopo kuanza kuwasaka kwa nguvu.
“Katika msako huu hatutamuacha mtu au mwajiri yeyote anayekiuka sheria iliyoanzisha Bodi ambayo inawapa mamlaka ya kufanya ukaguzi na ni kosa kisheria kwa mtu yeyote kuzuia ukaguzi huo,” alisema.
Alisema tayari wameongeza nguvu ofisi zao za Kanda zilizopo Mwanza, Arusha, Dodoma na Zanzibar ili kuendesha ukaguzi na msako katika mikoa yao na ile iliyo karibu nayo ili kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa ufanisi.
Akizungumzia hali ya ukusanyaji wa mikopo iliyoiva hadi kufikia Desemba 31, 2018, alisema kiasi cha Sh bilioni 85 kilikuwa kimekusanywa huku lengo la makusanyo kwa mwaka mzima wa fedha utakaomalizika Juni 30, 2018 ni Sh bilioni 130.
“Katika kazi hii ya ukusanyaji kwa miezi hii sita tumewabaini wanufaika wapya zaidi ya 26,000 na wameanza kulipa na kufanya jumla ya wanufaika wanaolipa hadi sasa kuwa zaidi ya 121,000. Nawashukuru sana waajiri wote wanaotimiza wajibu wao,” alisema.
Alibainisha changamoto wanazokutana nazo katika kazi ya ukusanyaji wa mikopo ni pamoja na baadhi ya waajiri, kutowasilisha kwa bodi ya mikopo orodha za waajiriwa ambao ni wahitimu wa taasisi za elimu ya juu kama sheria inavyotaka sambamba na kutowasilisha makato ya wanufaika kwa bodi kwa wakati.
Akizungumzia utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wahitaji kwa mwaka huu wa masomo 2017/2018, alisema jumla ya wanafunzi 122,623 wamepata mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 422.45.
Alisema waliopata mikopo kati yao wanafunzi 33,244 ni wa mwaka wa kwanza, waliopata mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 110.37 na wengine 89,379 ni wanaoendelea na masomo, ambao wamepata mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 312.16.
“Katika mwaka wa masomo uliopita 2016/2017 jumla ya wanafunzi 112,409 walipangiwa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 409.61 kati ya hao wanafunzi 28,383 walikuwa wa mwaka wa kwanza na wengine 86,688 walikuwa wanaendelea na masomo. Hata hivyo, aliwataka wanufaika wote kutoa ushirikiano katika kampeni hiyo na kujitokeza kurejesha mikopo hiyo ili kuepuka usumbufu.
Chanzo-Habarileo
Chanzo-Habarileo