Mwanafunzi wa darasa la sita Shule ya Msingi Vikonge Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi (14) ameuawa kikatili baada ya kubakwa kisha kuchomwa kisu ubavuni na kisha kunyofolewa sehemu za siri wakati akiwa anakwenda shuleni na mdogo wake aliyekuwa anasoma naye shule moja.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Katavi Damas Nyanda alisema tuki jana Januari 23,2018 majira ya saa moja na nusu asubuhi umbali wa kilometa moja na nusu kutoka katika shule ya msingi Vikonge.
Alisema siku hiyo ya tukio marehemu huyo alitoka nyumbani kwao kwa lengo la kwenda shuleni kama kawaida yake huku akiwa na mdogo wake wa kiume (11) mwanafunzi wa darasa la nne shule ya Msingi Vikonge ambaye jina lake limehifadhiwa.
“Wakati wakiwa njiani alitokea mwendesha pikipiki moja ambae walikuwa hawamfahamu na kusimamisha pikipiki yake na kisha aliwaambia awape msaada wa usafiri wa kuwafikisha shuleni kwao na baada ya kuambiwa hivyo wanafunzi hao walikubali kupewa msaada wa pikipiki”,alieleza.
“Hata hivyo mara baada ya marehemu kuwa amepanda pikipiki hiyo mwendesha boda boda huyo alimzuia mdogo wa marehemu asipande kwenye pikipiki hiyo na kisha aliiondoa kwa kasi huku akiwa na marehemu na kumwacha kaka yake”,aliefafanua Kamanda wa polisi.
Alisema hali hiyo ilimfanya kaka yake aamue kuifuata pikipiki hiyo kwa nyuma na ndipo wakati akiwa njiani aliona pikipiki kama ile iliyokuwa imembeba dada yake ikiwa pembezoni mwa barabara kwenye kichaka hata hivyo aliendelea na safari yake ya kwenda shuleni.
“Kaka huyo wa marehemu kutokana na kuwa na umri mdogo baada ya kufika shuleni hakuweza kumtafuta dada yake na badala yake aliingia darasani na kuendelea na masomo kama kawaida na baada ya muda wa masomo ilipofikia majira ya saa nane na nusu mchana alianza safari ya kurejea nyumbani pasipo kumtafuta dada yake”,alisimulia Kamanda huyo.
Kamanda Nyanda alieleza baada ya kuwa amefika nyumbani kwao wazazi wake walishtuka kumwona akiwa peke yake ndipo walipomuuliza aliko yake na ndipo aliwaeleza mazingira yote ya jinsi alivyo achana na dada yake wakati walipokuwa njiani na jinsi alivyoiona pikipiki iliyombeba dada yake ilivyokuwa kwenye kichaka.
Alisema baada ya kupata maelezo hayo, wazazi wa marehemu walipatwa na mashaka hivyo walimtaka mdogo wa marehemu awapeleke kwenye eneo aliloona pikipiki ikiwa kwenye kichaka.
“Wazazi wa marehemu waliokuwa wameongozana na majirani zao baada ya kufika kwenye eneo hilo walishtuka kuona majani yakiwa yamelala na walipoenda mbele kidogo waliuukuta mwili wa marehemu ukiwa amechomwa kisu sehemu ya ubavu wake wa kulia na sehemu za siri zikiwa zimenyofolewa”,alieleza Kamanda Nyanda.
Alisema jeshi la polisi mkoa wa Katavi linaendelea na msako wa kumtafuta mtu au watu waliohusika na mauaji hayo ya kikatili hadi sasa hakuna mtu wla watu waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Kaimu mwalimu Mkuu wa Shule ya Vikonge Mwalimu Gadinendi Kaseka ameiambia Malunde1 blog kuwa mpaka walipomaliza masomo ya siku hiyo hawakuwa na taarifa juu ya kifo cha mwanafunzi huyo ila walipata taarifa hiyo siku hiyo hiyo majira ya saa kumi na mbili jioni baada ya mwili wa marehemu kupatikana.
Na Walter Mguluchuma – Malunde1 blog