Mbunge wa Iramba Magharibi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amesema atawashangaa sana kuona wananchi wa jimbo la Kinondoni wakimpigia kura mgombea wa CHADEMA Salum Mwalimu kwa madai Ilani inayofanya kazi ni moja tena ya CCM.
Mhe. Mwigulu ameeleza hayo jana wakati wa akizindua kampeni hizo za uchaguzi mdogo katika Jimbo la Kinondoni ambapo upande wa CCM wamemsimamisha mgombea Mtulia Said Maulid ambaye hapo awali yeye ndiye alikuwa Mbunge wa Jimbo hilo kupitia CUF kabla hajajivua unachama wake na kuenda kumuunga mkono Rais Magufuli katika kujenga Taifa la Tanzania.
"Msije mkaenda kupiga kura ya uchaguzi mdogo kwa kiwango cha uchaguzi mdogo, twendeni tukapige kura kwa uzito ule ule kwamba ni jambo la msingi, la kitaifa na jambo la chama chetu lenye maslahi mapana nalo. Tutakapo tawanyika hapa kila mmoja awe kampeni meneja wa mgombea wetu na aje na wapiga kura siku hiyo ya kupiga kura", alisema Mwigulu.
Pamoja na hayo, Mwigulu amedai CCM inasababu zote za kushinda uchaguzi huo mdogo wa marudio kwa sababu Ilani inayotekelezwa ni moja ambayo ni CCM na itaishi mpaka 2020.
"Leo hii ukifuata uhalisia sababu zote za msingi za ushindi tunazo sisi lakini wao watabaki na moja tu kwamba kwa nini Mtulia alihama. Ilani ya uchaguzi iliyochaguliwa ni ya CCM na itatekelezwa hadi mwaka 2020, asitokee mtu ambaye atawadanganya, kumpigia kura mtu wakati hana ilani inayotekelezeka ni sawa na kupigia kivuli wakati kuna mtu", alisisitiza Mwigulu.
Kwa upande mwingine, Mhe. Mwigulu amewasii wananchi wa jimbo hilo kuwa makini wasije kudanganywa na mtu yeyote kwamba ana sera nzuri kwa sababu hakuna sera nyingine inayotekelezwa zaidi ya CCM.