Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack amefanya ziara ya kukagua baadhi ya mashamba ya watumishi wa halmashauri wa manispaa ya Shinyanga pamoja na wakulima na kukumbana na changamoto ya wadudu waharibifu (Viuwajeshi vamizi) ambao wanashambulia wa mazao na kutishia wakulima kukosa mavuno mazuri.
Mkuu huyo wa mkoa amefanya ziara ya kukagua mashamba hayo katika kata ya Mwasele,Lubaga, Chibe ,Kambarage na Mwamalili na kujionea baadhi ya watumishi wa serikali walivyojikita kwenye kilimo na kuonyesha mfano wa kilimo cha kisasa kwa wananchi ambao nao wamelima mazao mbalimbali na kutarajia kupata mavuno mengi lakini wadudu hao ndio imekuwa kikwazo kwao.
Mkuu wa mkoa alikuwa ameambatana na mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro,Naibu Meya wa manispaa ya Shinyanga Agnes Machiya na Mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga,Geofrey Mwangulumbi.
Akizungumza wakati akikagua mashamba hayo jana Januari 23,2018 Telack aliwataka wananchi kuendelea kuzitumia mvua zinazonyesha kwa kulima mazao ya chakula na biashara likiwemo zao la pamba kwa wingi ili baadae waje kupata vyakula vya kutosha pamoja na kuuza mazao yao ambayo yatawainua kiuchumi.
Alisema licha ya kuwepo na changamoto hiyo ya wadudu waharibifu ambao wanashambulia mazao kwa fujo, serikali imeshafanya jitihada za kutafuta ufumbuzi wa dawa ambayo itawaangamiza wadudu hao kutoka wizara ya kilimo, na wameshapewa kuonyesha mfano kwa wakulima ambayo ndiyo itatumika kuteketeza wadudu mashambani.
“Tayari hapa nina dawa ambayo nimepewa na Waziri wa Kilimo inaitwa (Duduba) ambayo hii ndiyo itatumika kuteketeza wadudu hawa (Viwajeshi vamizi) na kunusuru mazao ya wakulima kutoendelea kushambuliwa tena”, alisema.
Pia aliwaagiza maofisa kilimo wote kutoka ngazi ya kata hadi mkoa kutoa elimu kwa wakulima namna ya kutumia dawa hiyo Duduba, pamoja na namna ya kupulizia mazao yao, ilikutowapa tena nafasi wadudu waharibifu kushambulia mazao mashambani.
Nao baadhi ya wakulima ambao walifanikiwa kutembelewa mashamba yao kilio chao kikuu kilikuwa ni hao wadudu ambao wameonekana kuwa tishio kwa kushambulia mazao, na kuhofia huenda wakaambulia kuvuna mabua ama mavuno kidogo, na kuendelea kukabiliwa na janga la njaa licha ya kujituma kwenye kilimo.
Mmoja wa wakulima hao kutoka kata ya Chibe Sangulwa Dili alisema wadudu hao ni hatari licha ya kupulizia dawa wamekuwa hawafi, na kuitaka Serikali pia iwapatie elimu ya kitaalamu namna ya kupulizia dawa iliwapate kuwa angamiza wadudu hao na kunusuru mazao yao.
Naye Ofisa kilimo kata ya Kambarage Matrida Magalata, alisema pia kwa wakulima ambao hawatoweza kununua dawa hiyo ya Duduba, wanaweza kutumia njia ya kienyeji kuua wadudu hao kwa kuchanganya majivu kilo mbili pamoja na kuweka vijiko vitatu vya pilipili ya unga , na kisha kunyunyuzia juu ya tawi la zao mahari ambapo wadudu hao hushambulia, na wataweza kufa papo hapo.
Alisema njia hiyo ni ya kienyeji tayari ameshaijaribu kwenye baadhi ya mashamba na imefanikiwa kuua wadudu hao Viwajeshi Vamizi, na hivyo kutoa wito kwa wakulima ambao hawatakuwa na uwezo wa kununua dawa za kitaalamu pia wanaweza kutumia njia hiyo.
Kwa upande wake Ofisa kilimo wa halmashauri ya mansipaa ya Shinyanga Rajabu Masenche, alisema katika halmashauri hiyo kunajumla ya wakulima 29,800 kutoka vijiji 17,na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kufuata ushauri wa wataalamu wa kufuata kilimo cha kisasa ambacho kitawapatia mavuno mengi.
ANGALIA PICHA HAPA
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akiwa na wakulima wa kata ya Chibe wakiangalia jinsi wadudu waharibifu wanavyoshambulia mazao.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga akiangalia mahindi yaliyoshambuliwa na wadudu
Mmoja wa wadudu waharibifu wanaofahamika kwa jina la Viwajeshi Vamizi akishambulia mazao
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro aking'oa shina la zao ambalo limeshambuliwa nawadudu waharibifu ili lisiweze kusambaza wadudu hao kwenye mazao mengine.
Kulia ni Mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Geofrey Mwangulumbi akichimba shimo kwa ajili ya kufukia mashina ya mazao yaliyokwisha shambuliwa na wadudu hao.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack akionyesha dawa ambayo amepewa na Waziri wa Kilimo, inaitwa Duduba ambayo ndiyo inafaa kuteketeza wadudu hao Viwajeshi Vamizi, na kuagiza Maofisa Kilimo wote wawaambie wakulima kutumia dawa hiyo pamoja na kuwaelekeza namna ya kuitumia ili kunusuru mazao yao yasiendelee kushambuliwa.
Ofisa mkaguzi mimea na mazao kutoka ofisi ya Kanda ya Magharibi Shinyanga akionyesha jinsi wadudu wanavyoshambulia pia zao la pamba
Naibu Meya wa manispaa ya Shinyanga Agnes Machiya akiangalia wadudu jinsi walivyoshambulia zao la pamba
Wa pili kushoto ni Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga Agnes Machiya akifuatiwa na mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro wakitoa hamasa kwa wakulima kwa kupalilia shamba la pamba ambalo ni la viongozi wa serikali kata ya Chibe
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro katikati akiendelea kulima akiwa na wakulima wa kata ya Chibe
Kushoto ni Afisa Mtendaji wa kata ya Kambarage James Dogani akimuonyesha mkuu wa wilaya Josephine Matiro na Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack mashamba yake ya mazao ya chakula na biashara
Mazao ya chakula cha mahindi yakiwa baadhi yameshambuliwa na wadudu waharibifu.
Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog