Shekhe Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakar Zuberi, ametaka viongozi wa dini nchini kuheshimiwa na jamii ikiwemo kutekelezewa mahitaji yao ya msingi ili waweze kujikimu kimaisha.
Akizungumza na waumini wa dini hiyo Jumamosi Januari 6 katika mhadhara wa Maulidi uliofanyika katika kata ya Mazingara wilayani Handeni mkoani Tanga, Mufti Zuberi amesema kila kiongozi duniani amewekwa na Mungu hivyo ni lazima aheshimiwe.
Amesema kuna baadhi ya watu wamekuwa na tabia ya kudharau viongozi wao kwa kuwatolea lugha chafu na zenye maudhi kwa kujionyesha wana uelewa kuliko viongozi.
"Viongozi lazima waheshimiwe kwa namna yoyote ile, sisi viongozi wa dini ndio tunaosababisha kuwepo amani na utulivu pia kutoa vizazi vyenye elimu ya dini kwa kuwafundisha watoto imani," alisema na kuongeza:
"Lazima sasa tuheshimiwe, iwe shehe au kiongozi wa dini nyingine na pia wa serikali ambao ndio wanasababisha mipango yetu ya kidunia inakwenda sawa. Kiongozi yoyote anateuliwa na Mungu na sio binadamu hivyo kuheshimiwa ni lazima."
Mhibiri wa dini ya Kiislamu kutoka jijini Dar es Salaam, Shehe Yusuph Hossein, amesema waumini wa dini hiyo wanatakiwa kufuata maagizo na mafundisho aliyoacha Mtume Muhammad kwani bila kufanya hivyo maovu hayatakwisha.
Ameongeza kuwa maadili katika jamii yameshuka kwa sababu watu wameacha kufuata maagizo ya dini zao badala yake wametawaliwa na Dunia ambayo imejaa maovu.
Alipokaribishwa asalimie hadhara hiyo, Mbunge wa Jimbo la Handeni Mjini, Omari Kigoda, akapendekeza kuwepo kwa utaratibu wa kudumu wa viongozi wa dini kukutana mara kwa mara na waumini wao ili kuweza kukumbushana mambo ya dini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Handeni, Athumani Malunda, amewapongeza walioandaa hadhara hiyo kwa kuifanya muda wa mchana kuliko ilivyozoeleka nyakati za usiku na kusema kuwa utaratibu huo ni mzuri kwa usalama wa raia, mali zao na viongozi wanaofika kuhudhuria.
Social Plugin