Siku moja baada ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kutangaza kuanza kampeni ya miezi mitatu ya kuwasaka wanufaika wa mikopo ambao mikopo yao imeshaiva, wadaiwa wameanza kumiminika kuulizia taratibu ya urejeshaji.
Kaimu Mkurugenzi wa Habari wa HESLB, Omega Ngole amesema tangu kusambaa kwa taarifa hiyo hapo jana Jumatano amekuwa akipigiwa simu na wanufaika wengi wakihitaji kufahamu taratibu.
Amesema miongoni mwao ni pamoja na wale walio nje ya ajira lakini tayari mikopo yao imeshaiva na inatakiwa kuanza kulipwa (mikopo iliyoiva ni ile iliyotimiza miezi 24 baada ya kumaliza chuo).
“Hadi kufikia saa tisa jioni(leo Alhamisi) tutakuwa na namba ya wanufaika waliojitokeza kuanza kulipa, kupunguza baada ya kupata taarifa ya kuwepo kwa msako huo maalumu, unaotarajiwa kuanza Jumatatu ya wiki ijayo,” amesema Ngole.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema utaratibu kwa waliokuwa nje ya ajira tayari umeandaliwa.
“Wakifika katika ofisi zetu za kanda ambazo tumeziboresha watakuta utaratibu namna ambavyo wanaweza kulipa madeni yao, ” amesema Razaq Badru.
Razaq Badru pia amezungumzia wanufaika ambao madeni yao yameiva na wapo nje ya nchi, kuwa kuna madawati maalumu kwa ajili yao yameandaliwa kila kanda.
“Hakuna atakayeachwa katika kulipa madeni haya, waliopo nje wana madawati yao na tunafanya kazi kwa kushirikiana na wizara ya mambo ya nje na balozi za nchi husika ili kuhakikisha wanalipa mikopo yote iliyoiva, ” amesema Razaq Badru.
Social Plugin