MILA na desturi zilizojengeka katika jamii ya Kimasai ya kutowajengea watoto wa kike na wa kiume makazi rasmi ya kudumu katika kaya zao zimedaiwa kuchangia ngono katika umri mdogo na mimba za utotoni.
Hayo yalisemwa na washiriki wa warsha ya elimu ya afya ya uzazi na elimu kwa mtoto wa kike wilayani Ngorongoro.
Warsha ya elimu ya uzazi na elimu kwa wasichana inaendeshwa na Shirika la Umoja la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kuwajumuisha washiriki zaidi ya 60 wakiwemo wanafunzi, akina mama, walimu na maofisa wa elimu na afya wilayani Ngorongoro.
Mama wa Kimaasai Nambaso Sayori akichangia jambo baada ya mwanafunzi kuwasilisha kazi kikundi kuhusu mzunguko wa Hedhi ya mwanamke. Sayori alisema ni muhimu kwa elimu hiyo kuwapatia wasichana ili waweze kujielewa kwa sababu wao kama kizazi kilichopita hawakupata nafasi ya mafunzo kama hayo.
Lengo la warsha hiyo ni kutoa elimu rika ya afya ya uzazi na elimu kwa mtoto wa kike ili kufanikisha malengo yao ya maisha.
Washiriki hao walisema kwa mujibu wa desturi na mila, watoto wa kike na wa kiume huwa hawana mahali rasmi na salama pa kulala mara wanapokuwa wamebalehe kwa kuwa hulazimika kuondoka kwenye boma.
Washiriki hao wamesema mara baada ya giza linapoingia, kumaliza kazi na kula chakula cha usiku, vijana huondoka nyumbani na kwenda mahali popote ambapo anaweza kupata mahali pa kulala bila wazazi kujali alikolala na wala hawaulizwi wamelala wapi na iwapo ni salama.
Washiriki kutoka shule tatu za sekondari na moja ya msingi wilayani Ngorongoro wakisikiliza kwa makini mada inayohusu afya ya Uzazi katika mafunzo ya stadi za Maisha kuhusu Afya ya Kujamiiana na Uzazi iliyofanyika katika shule ya Sekondari ya Loliondo tarehe 08 hadi 13 Desemba 2017 na kuendeshwa na Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO). Mafunzo hayo yaliwashirikiwa wanafunzi, akina mama, walimu, viongozi wa wilaya kutoka sekta za elimu na afya na waandishi wa habari. Lengo la mafunzo hayo ni kuunda Vikundi vya Vijana katika shule na Akina Mama vitakavyotayarisha Vipindi vinavyohusu masuala yao.
Mara nyingi, washiriki hao wameongeza, kwa kuwa huwezi kulala mahali pamoja kila siku kutokana na mwendelezo wa mila hiyo, vijana huishia katika ngoma za usiku zijulikanazo kama ‘esoto’ na ndiko vishawishi vya ngono vinapotokea.
Kwa kuwa akinamama ndio wanaojenga nyumba (boma) za Kimaasai, vijana wameombwa kujenga mazingira mazuri katika maboma yao kuhakikisha kuwa kunakuwa na nyumba ambayo itajengwa mbali na pale wanapolala wazazi ili kudumisha mila, lakini pia kulinda utu wa mtoto wa kike.
Mimba za utotoni katika jamii ya Kimaasai zinaongezeka kwa kasi pamoja na mambo mengine ni kutokana na tamaa ya mali, mila na desturi ya kutowapatia wasichana mahali maalum pa kulala usiku.
Akina Mama wa Kimaasai wakibadilishana mawazo kuhusu somo la afya ya Uzazi na mahusiano yake na ukeketaji, wakati mwanafunzi wa darasa la tatu kutoka Shule ya Msingi ya Ololosokwan Ana Alais akishiriki katika mjadala huo. Kipindi cha mazoezi cha kuendesha mahojiano kwa ajili ya kupata habari kati ya Mtangazaji wa Redio Jamii Loliondo, Mako Kibaki na mmoja wa washiriki wa akina mama Melora Naingisa. Mahojiano hayo ni miongoni mwa vielelezo katika mafunzo ya Elimu ya Kujamiiana na Uzazi iliyofanyika Micheweni, Pemba yenye lengo la kuwapa ujuzi stadi wanafunzi wa shule tatu za sekondari na moja ya msingi na kikundi cha akina mama Wilayani Loliondo kutayarisha Vipindi vya redio vinavyohusu masuala yao.