WAFAHAMU WANAFUNZI BORA KITAIFA WALIOTIKISA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2017..YUMO ELIZABETH NA ANNA




Mwanafunzi aliyeshika nafasi ya pili katika matokeo ya Mtihani wa kidato cha nne kutoka Shule ya Marian Girls ya Bagamoyo,Elizabeth Mangu(kulia) akipongezwa na Mama yake mzazi Wande Mandalu eneo la Kirumba Valley Christian Center jijini Mwanza baada ya kupata matokeo yake.Picha na Michael Jamson 
Mwanafunzi aliyeshika nafasi ya tatu kitaifa Anna Mshana kutoka shule ya wasichana ya Marian Girls. 

***

Leo Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne 2017 ambapo mwanafunzi aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa ni Felison Mdee kutoka Marian Boyz,huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Elizabeth Mango kutoka Marian Girls na nafasi ya tatu ikichukuliwa na Anna Benjamin Mshana pia kutoka Marian Girls..Soma zaidi <<Hapa>> 

WASHINDI WASIMULIA SIRI YA MAFANIKIO

Elizabeth Mangu, mshindi wa pili Kitaifa katika mitihani ya kidato cha nne amesema kumtanguliza Mungu katika kila kitu, ndoto ya kuwa wa kwanza, bidii kwenye masomo na usimamizi wa karibu wa wazazi na walimu ndiyo siri ya mafanikio yake.


Akizungumza katika mahojiano maalum jijini Mwanza leo Januari 30, Elizabeth amesema tangu alipojiunga kidato cha kwanza, alijiwekea lengo la kushika nafasi ya kwanza katika mitihani ya Taifa na aliwafuata walimu wake kuomba ushauri wa kufanikisha lengo hilo.

“Niliweka lengo la kushika nafasi ya kwanza kama alivyofanya Robina aliyeongoza mitihani ya kitaifa akitokea shule yetu ya Marian Girls; nilimfuata Mwalimu wa taaluma Ihonde na mwenzake wa Civics anayeitwa Mwanduzi kuwaomba ushauri wa kufanikisha hilo,” anasema na kuongeza

“Wote walinishauri kuzingatia masomo, kusoma pamoja na kusaidia wenzangu darasani kama njia ya kujifunza, kuzingatia maelekezo ya walimu na wazazi shuleni na nyumbani pamoja na kumcha Mungu kama mwanzo wa hekima,”

Akizungumza mbele ya mama yake mzazi, Wande Mandalu ambaye ni mwalimu katika shule ya Sekondari ya Kiloleli jijini Mwanza, Elizabeth alisema mwongozo na ukali wa wazazi wake aliposhuka kitaaluma pia imesaidia mafanikio yake.

“Nawashauri wazazi wawe karibu na kufuatilia mienendo ya watoto wao kuanzia nyumbani hadi shuleni na kuwatia moyo wanapofanya vema bila kuacha kuwaonya na kuwakaripia wanapokosea,” amesema

Kauli hiyo iliungwa mkono na mama yake, Wande Mandalu pamoja na Mwalimu wake wa masomo ya dini katika Kanisa la KVCC, Geofrey Lugwisha waliosema liha ya kuwajenga watoto katika imani ya kiroho, wazazi wana wajibu wa kuwasaidia watoto wao kielimu, kuwapongeza na kuwaonya wanapopotoka.

“Wazazi lazima tuwe wasimamizi wa karibu kwa kufuatilia nyendo za watoto kuanzia nyumbani, shuleni hadi mitaani; lazima wajua ratiba na kuwapa miongozo inayofaa maishani, hasa msisitizo kwenye elimu ambayo ndio urithi wa kudumu,” amesema Mwalimu Mandalu, mama wa watoto watatu

Eliza ni mtoto wa pili katika familia yake ya watoto watatu akitanguliwa na kaka yake Joseph Mangu na mdogo wake, Carren Mangu aliyesoma kidato cha kwanza shule ya wasichana ya Marian.

MSHINDI WA TATU KITAIFA NAYE ALONGA

Naye Mwanafunzi aliyeshika nafasi ya tatu kitaifa Anna Mshana kutoka shule ya wasichana ya Marian iliyoko Mkoa wa pwani amesema mtoto wa kike ana uwezo wa kufanya vizuri kimasomo kama atajituma zaidi na kuacha uvivu.

Anna ambaye ameonekana mwenye furaha baada ya kushika nafasi hiyo ambayo hakuitarajia amesema siri ya mafanikio yake ni kujituma na kujiongeza bila kutegemea kila kitu kutoka kwa mwalimu.

"Kwanza tulisikia asubuhi kuwa matokeo yametoka, na tukaambiwa kuwa tumefaulu vizuri na shule yetu imeingia katika kumi bora, lakini furaha iliongezeka zaidi nilivyoambiwa kuwa nimekuwa wa tatu kitaifa," amesema.

Amesema ndoto yake ni kuwa mhandisi kwani mbali na kuwa alisoma masomo yote lakini alibobea zaidi katika masomo ya sayansi.

Amesema pia mafanikio yake kimasomo yametokana na jitihada pamoja na sala kwani hakuna mafanikio bila jitihada na kumtanguliza Mungu.

"Nilikuwa nafanya vizuri, lakini kutokana na msukumo kutoka kwa wazazi wangu imenifanya niwe nafanya vizuri kila siku, hivyo nilikuwa nasali kila mara," amesema.

Anna amewashukuru wazazi wake kwa ushirikiano wao mzuri, walimu na wanafunzi wenzake hata hivyo amesema matokeo hayo sio mwisho wa safari yake kwani ana safari ndefu kimasomo.

Mama mzazi wa Anna Zamara Hassani amesema matokeo hayo ni mwanzo mzuri kwa binti yao kwani jitihada zao ni kuhakikisha anasoma na kufaulu, vizuri masomo yake.

"Yaani tulifurahi sana, baada ya kusikia kuwa Anna ameshika nafasi ya tatu kitaifa, tulikuwa tunajua kuwa atafaulu lakini hatukuwaza yeye kuwa watatu," amesema.

Baba mzazi wa Anna Benjamini Mshana amesema amefurahishwa na matokeo hayo hivyo amemtaka binti yake kuongeza juhudi zaidi.

"Mzazi ukimsimamia vizuri mwanao ana nafasi nzuri ya kufanya vizuri, mimi ni mwalimu najua umuhimu wa mzazi kumsimamia mwanafunzi kwani yeye hawezi, kujisimamia mwenyewe," ameongeza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post