WANANCHI WAVAMIWA BAA NA WATU WALIOVAA SARE ZA ASKARI MAGEREZA,WAPIGWA NA KUPORWA SIMU,FEDHA




Watu zaidi ya 10 wakiwemo waliovaa sare za askari Magereza wamevamia baa moja iliyopo Keko jijini Dar es salaam, kujeruhi watu huku wakipora mali mbalimbali zikiwamo simu za mkononi na fedha za wateja.

Watu hao walivamia baa hiyo  iitwayo Omax jana saa tano usiku na kuanza kuwapiga na kuwapora mali hizo wateja kisha kutokomea gizani.

Awali, kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Lukula alisema alipopigiwa simu na mwandishi wa habari hizi, alisema yuko Kibiti kikazi. Hata hivyo alikiri kupigiwa simu usiku wa siku ya tukio na watu wakitaka kupatiwa fomu za PF3 kwa ajili ya matibabu.

 “Nilipigiwa simu na watu wengi wakitaka kupatiwa PF3 wameumia, nikawaambia niko mbali waende tu Kituo cha Polisi Chang’ombe watasaidiwa, sasa sijui walienda ama vipi na sasa hivi siwezi kutoa ufafanuzi kwa sababu niko Kibiti kikazi,” alisema.

Mkuu wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Dar es Salaam, Agustine Mboje alisema taarifa ya kuvamiwa kwa baa na watu kupigwa hana, lakini anachofahamu kuna askari wao alivamiwa na vibaka na kupigwa wakati akienda kazini, kisha wakatoa taarifa Kituo cha Polisi Chang’ombe.

Mboje alisema baada kutoa taarifa, polisi wakishirikiana na askari Magereza walifanya msako kuwatafuta na kuwakamata baadhi ya vibaka ambao waliwafikisha katika kituo hicho.

Mhudumu wa baa iliyovamiwa aliyejitambulisha kwa jina moja la Mary alisema walifika watu zaidi ya 10 wakiwa wameshika mikanda wakaanza kuwapiga watu, lakini alipoona hivyo alikimbilia chooni akiwa na mteja ambako walifuatwa na kuanza kupigwa.

Alieli Nelson aliyekuwa mteja ambaye alijeruhiwa kichwani, alisema walikuwa kwenye baa hiyo wakisubiri chakula na ghafla walivamiwa na kundi la watu wakiwa wamevalia sare za askari Magereza na wengine wakiwa wamevaa kiraia.

“Hapa nilipo nimepigwa vibaya, nimepasuliwa kichwa, nimeibiwa simu yangu pamoja na pesa Sh500,000 huku wakitutisha kwamba atakayeshtaki atafunguliwa kesi,” alisema Alieli.

George Cosmas alisema alivamiwa na kupigwa, lakini alishuhudia mmoja wa wateja wenzake akiumizwa mkono na kuporwa.

“Wamewapiga watu sana na kuwaibia vitu mbalimbali vikiwamo pesa na simu, pia kuna watu ambao ni raia wa Kongo wamepigwa na mmoja kuvunjwa mkono” alisema.

Akizungumzia tukio hilo, mmiliki wa baa hiyo, Gerald Temba alisema wakati wa tukio hakuwepo lakini alipigiwa simu akielezwa walikuwepo watu wavamizi wakiwemo waliovalia sare za Magereza waliokuwa wanapiga watu na kupora vitu.

Alisema baada ya kupewa taarifa alimpigia simu Kamanda Lukula kumfahamisha juu ya tukio hilo na kujibiwa kuwa taarifa zimeshamfikia. “Nilimpigia RPC wa Temeke kumfahamisha kwa nini tunavamiwa na kupigwa wakati leo ni sikukuu na muda wa kufunga ni saa sita, lakini alinijibu anayo hiyo taarifa,” alisema Temba.

Aliongeza kuwa katika tukio hilo alipata hasara ikiwemo viti, meza na chupa kuvunjika pamoja na wateja waliokuwemo kuondoka bila kulipa bili za vinywaji na chakula zinazofikia Sh300,000.

Na Fortune Francis, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post