Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemtolea uvivu mkuu wa wilaya ya Nyasa, Isabella Chilumba na mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Dk Oscar Mbyuzi, ambao wamekuwa wakivurugana, akisema tofauti zao zinaathiri watendaji walio chini yao na kuumiza wananchi.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu inasema kuwa Majaliwa alisema hayo alipokuwa katika ziara yake Wilaya ya Nyasa.
Waziri Mkuu alisema katika ziara zote za mikoani, amekuwa akipata malalamiko mengi kwenye halmashauri na mabaraza ya madiwani, lakini amekuta hali si shwari Wilaya ya Nyasa kwa kuwa kuna migogoro midogo kwenye uongozi wa juu.
“Tatizo ni dogo huku juu, bado mnavurugana mkuu wa wilaya na mkurugenzi. Ninyi ni viongozi wa juu, acheni kuvurugana, fanyeni kazi. Mkigombana wanaoumia ni wananchi,” alisema.
“Mkuu wa wilaya anaweza kuingia kwenye kikao chochote cha halmashauri na kudai apewe taarifa, mpeni. Yeye siyo mjumbe wa kikao hicho, lakini anayo mamlaka ya kushiriki.
“Mkurugenzi ni mtendaji mkuu, tumekukabidhi watumishi uwaongoze. Tumekukabidhi fedha kwa ajili ya maendeleo ya wilaya hii. Mtu akizitamani, mwambie hizi fedha zina maelekezo rasmi, hazipaswi kwenda kokote.”
Aliwataka madiwani wasijenge tabia ya kuongeza siku za vikao kwa makusudi ili tu wapate posho za ziada.
“Msitengeneze siku za ziada na kumpa presha Mkurugenzi. Kama kikao ni cha siku moja, basi kiishe. Siyo kulaza ajenda ili mmalizie kesho yake. Mkurugenzi akiwanyima fedha, msianze kugombana naye kwa sababu yeye hana fedha za kumgawia mtu,” alisisitiza.