Wimbo wa Papa ulioimbwa na msanii Gift Stanford ‘Gigy Money’ na ule wa Wowowo ulioimbwa na Zaiid Yao, umeibua mjadala katika kikao cha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na viongozi wa vyama na mashirikisho ya wasanii.
Leo Ijumaa, Waziri Mwakyembe alikutana na viongozi kwa ajili kujadili suala la maadili ya mavazi katika tasnia hiyo kwenye ukumbi wa Uwanja wa Taifa ikiwa ni siku chache tangu Rais John Magufuli akemee suala hilo na kutaka watakaovaa vibaya kazi zao zipigwe marufuku na vituo vya televisheni vitakavyoonesha kufungiwa.
Wakati Waziri akiwa anaelekeza zaidi mjadala katika kikao hicho kwa upande wa video, kukaibuka hoja kwamba hata maudhui yanayoimbwa kwenye nyimbo za sasa hivi sio.
Aliyetoa hoja hiyo alikuwa ni Mjumbe wa Chama cha Muziki Dansi(Chamudata), John Kitime ambaye alisema wakati wanajadili mavazi pia waangalie na suala zima la maneno yanayoimbwa ndani ya nyimbo hizo huku akitolea mfano wa wimbo wa ‘Papa’.
Mbali na viongozi hao kunyooshea kidole kwa wimbo wa Papa ambao umejizolea umaarufu, pia video ya wimbo wa Wowowo nao umeonekana kuwa gumzo katika kikao hicho, ambapo hata hivyo zote hizo Waziri alionekana kutozijua.
Katika wimbo wa Papa, kwa nyakati tofati Gigy akihojiwa anasema yeye amemaanisha samaki na sio kama ambavyo watu wanafikiria.
Wakati kwa video ya wimbo wa Wowowo imeonyesha maungo ya mwanamke yakiwa katika mavazi yasiyofuata maadili ya Kitanzania.
Hata hivyo Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godifrey Mngereza alipobanwa na Waziri kueleza kama kuna sheria mahususi za za kuwabana wasanii katika mavazi, amesema ni kama hazipo ijapokuwa wamekuwa wakiwasisitiza wasanii mara kwa mara kuvaa nguo zinazositiri maungo na kukubalika katika tamaduni za Kitanzania.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Joyce Fisoo, amesema ili kudhibiti mambo hayo ya mavazi kwa wasanii, ipo haja ya vituo vya TV ambavyo vimekuwa vikizionesha kuzihariri kabla hazijarushwa na kwa watakaoonekana wakaidi basi kazi zao zikataliwe.
Mwanamuziki Wastara Thomas ambaye ni mmoja wa wajumbe katika kamati ya maadili ya muziki wa Bongo Fleva, amesema hatua iliyofikiwa na serikali ya kukutana na viongozi kujadili suala la mavazi ni zuri kutokana na ugumu waliokuwa wanaoupata katika kuwakemea waliokuwa wanaenda kinyume.
“Labda kwa kuwa sasa hivyo serikali imeliona suala hilo na kuingilia kati, hata kamati yetu itakuwa na nguvu ya kuwachukulia hatua ambao wamekuwa wakiyafanya haya kwa kuwa wengi huko nyuma walikuwa wakiidharau kamati,” amesema Wastara.
Na Nasra Abdallah, Mwananchi
Social Plugin