Kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu Acacia kupitia migodi yake ya Buzwagi na Bulyanhulu imekabidhi hundi za shilingi bilioni 1.1 kwa halmashauri ya wilaya ya Mji wa Kahama na Msalala mkoani Shinyanga kwa ajili ya malipo ya ushuru wa huduma kwa kipindi cha Mwezi Julai hadi Disemba mwaka 2017.
Acacia imekabidhi hundi ya shilingi milioni 924,881,819.78 kwa halmashauri ya wilaya ya Mji wa Kahama zilizotolewa na mgodi wa Buzwagi na hundi ya shilingi milioni 153,591,456 kwa halmashauri ya wilaya ya Msalala zilizotolewa na mgodi wa Bulyanhulu na kufanya jumla kuwa shilingi bilioni 1.1.
Meneja Mkuu wa migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu,Benedict Busunzu amekabidhi hundi hizo kwa mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurulu leo Alhamis Februari 8,2018 mjini Kahama.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo,Busunzu alisema mgodi wa Bulyanhulu pia ulipa shilingi 75,649,524 kwa halmashauri ya wilaya ya Nyang’wale mkoani Geita ikiwa ni sehemu ya ushuru wa huduma kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Disemba 2017.
Busunzu alisema kupungua kwa uzalishaji katika migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu kumesababisha kupungua kwa kiwango cha uchangiaji wa ushuru wa huduma katika miezi sita iliyopita ikilinganishwa na mwaka jana na mwaka juzi.
Hata hivyo alisema Acacia imedhamiria kuendelea kuwa mdau mkubwa wa maendeleo kwa kuendelea kusaidia maendeleo ya biashara za wazawa pamoja na kushirikiana na serikali katika miradi endelevu ya muda mrefu kwenye jamii.
Busunzu alieleza kuwa Acacia inaendelea kushirikiana na serikali ya mkoa na wilaya katika kutekeleza miradi miwili mikubwa ya miundombinu ya jamii katika eneo la maji na afya.
“Bulyanhulu itafadhili shilingi bilioni 1.1 kwenye awamu ya pili ya kuboresha kituo cha afya cha Bugarama ili kuwezesha kufikia hatua ya kuwa hospitali ya wilaya,pia tumechangia shilingi bilioni 4.5 katika mradi wa ushirikiano wa Maji kutoka Ziwa Victoria katika halmashauri ya Msalala na Nyang’wale”,aliongeza Busunzu.
Naye Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu aliishukuru Acacia kwa kutoa ushuru wa huduma na kuwaomba kuendelea kushirikiana na halmashauri za wilaya katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Nkurlu aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri kutumia vizuri pesa zilizotolewa na Acacia ili zitoe matokeo chanya ikiwemo kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Kahama,Underson Msumba alisema watazitumia pesa hizo kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo kuboresha huduma za afya wilayani humo.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Katikati ni Meneja Mkuu wa Migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu Benedict Busunzu akikabidhi hundi ya shilingi153,591,456 kwa Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu kwa ajili ya malipo ya ushuru wa huduma kwa halmashauri ya wilaya ya Msalala katika kipindi cha mwezi Julai hadi Disemba 2017. Kulia ni Meneja wa Huduma na Mahusiano wa Acacia, Elias Kasitila.Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu akikabidhi hundi hiyo ya shilingi milioni 153 kwa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Msalala Simon Berege
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkuru,Meneja mkuu wa migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu Benedict Busunzu,Meneja wa Huduma na Mahusiano wa Acacia, Elias Kasitila na Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Msalala Simon Berege wakiwa wameshikilia hundi ya shilingi milioni 153.
Katikati ni Meneja Mkuu wa Migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu Benedict Busunzu akikabidhi hundi ya milioni 924,881,819.78 kwa Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu kwa ajili ya malipo ya ushuru wa huduma kwa halmashauri ya wilaya ya Mji wa Kahama katika kipindi cha mwezi Julai hadi Disemba 2017. Kulia ni Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Kahama,Underson Msumba
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu akikabidhi hundi hiyo kwa Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Kahama,Underson Msumba
Picha ya pamoja baada ya makabidhiano ya hundi mbili
Meneja Mkuu wa Migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu Benedict Busunzu akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhi hundi zenye jumla ya shilingi bilioni 1.1
Meneja Mkuu wa Migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu Benedict Busunzu akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema Acacia itaendelea kushirikiana na serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu akizungumza baada ya kupokea hundi zenye jumla ya shilingi bilioni 1.1 zilizotolewa na Acacia
Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Kahama,Underson Msumba.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog