Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoa wa Katavi inamshikilia Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kaulolo Tarafa ya Inyonga Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi Kevin Elick Malenge kwa tuhuma za kumkamata akipokea rushwa ya shilingi 150,000 kutoka kwa mkazi mmoja wa kijiji hicho ili aweze kumruhusu kuishi na kufanya kazi ndani ya hifadhi ya msitu.
Kaimu Kamanda wa TAKUKURU wa Mkoa wa Katavi Cristopher Nakua alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa jana majira ya saa nne asubuhi katika eneo la kijiji cha Kaulolo.
Alisema Mthumiwa Kevin alikamatwa kufuatia TAKUKURU kupatiwa taarifa kutoka kwa msiri wao kuwa afisa mtendaji huyo ameomba kiasi cha Tshs 200,000 kwa msiri huyo ili aweze kumwingiza ndani ya hifadhi ya msitu ulipo kwenye kijiji hicho ili aweze kuishi huko na kufanya shughuli za kilimo .
Nakua alieleza kuwa baada ya TAKUKURU kupata taarifa hizo ilianza kufanya uchunguzi na kubaini kuwa afisa mtendaji huyo amekuwa akijihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa kwa watu mbalimbali kwa kupokea kiasi cha kati ya Tshs 150,000 na Tshs 200,000 kwa lengo la kuwaingiza watu kuishi ndani ya hifadhi ya msitu kinyume na sheria.
Baada ya TAKUKURU kubaini mpango huo wa Afisa mtendaji wa Kijiji kuomba apatiwe rushwa ya shilingi 200,000 ndipo jana walipofanikiwa kumkamata mtuhumiwa akiwa katika eneo la tukio akipokea rushwa ya Tshs 150,000.
Alisema baada ya mtuhumiwa kukamatwa akipokea fedha alichukuliwa na maafisa wa TAKUKURU kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Kaimu Kamanda Nakua alisema mtuhumiwa alikiri kupokea rushwa hiyo na uchunguzi umekamilika sasa anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa ili kujibu tuhuma zinazomkabii.
Katika hatua nyingine Kaimu Kamanda Nakua ametoa wito kwa jamii kutojihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea au kutoa rushwa na haitasita kuwachukulia hatua wale wote watakaojihusisha na vitendo vya rushwa hasa viongozi waliopewa thamana na serikali kulinda rasilimali za Taifa na hifadhi zetu, kwa kufuata kanuni taratibu na sheria za nchini.
Na Walter Mguluchuma - Malunde1 blog