Raia wa Nigeria, Christian Ugbechi (26) aliyekamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) baada ya kukutwa na pipi 59 za dawa za kulevya aina ya Cocaine, jana Januari 31, 2018 ametoa pipi nyingine 23.
Ugbechi alikamatwa Januari 29, 2018 akiwa anasafirisha dawa hizo za kulevya kwenda nchini Ufaransa, huku akiwa ameficha pipi 59, kati ya hizo 56 alizificha kwenye soksi iliyokuwa katika begi lake la mgongoni, tatu alizitoa kwa njia ya haja kubwa.
Baada ya kudakwa, alikiri kuwa na pipi nyingine tumboni lakini leo Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Matanga Mbushi ameliambia Mwananchi kuwa mtuhumiwa huyo ametoa pipi nyingine 23, kufanya idadi yake kuwa pipi 82.
“Kwa maelezo ya mtuhumiwa anadai ameshamaliza kuzitoa pipi zote tumboni lakini tunaendelea kumuweka chingi ya uangalizi maalum,” amesema Mbushi na kuongeza,
“Bado tunamfuatilia kwa maana ya kila anapokwenda haja kubwa, lengo ni kujipa uhakika kama kweli amemaliza pipi hizo.”
Na Pamela Chilongola,Mwananchi
Social Plugin