Bunge limeitaka serikali kuhakikisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anafanya ukaguzi wa kiuchunguzi na kiufanisi katika mikataba yote inayohusu mradi wa Mlimani City na kuwasilisha ripoti bungeni, baada ya kubaini dosari kubwa kwenye uendeshaji wa mradi huo.
Agizo hilo limetolewa ikiwa ni wiki mbili baada ya chombo hicho cha kutunga sheria kuukagua mradi huo jijini Dar es Salaam.
Katika ukaguzi wake, Bunge liligundua mbia wa mradi huo unaokihusisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amewekeza mtaji wa Dola za Kimarekani 75 (Sh. 150,000) kutoka mfukoni kwake.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka, ndiye alitoa agizo kwa CAG kukagua mradi huo alipowasilisha bungeni mjini hapa jana taarifa ya shughuli za kamati yake kwa mwaka 2017.
Alisema upungufu uliobainika katika mradi huo unainyima serikali mapato stahiki na hivyo kuwa eneo mojawapo lenye matumizi mabaya ya fedha za umma.
Kaboyoka alisema kamati yake imebaini dosari kutokana na mradi wa ujenzi wa Mlimani City ulioanza Oktoba mosi, 2004 ukitakiwa kukamilika Septemba mosi, 2006 kwa makubaliano ya mkodishwaji na mkodishaji, kwa maana ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Kampuni ya Mlimani Holding Limited (MHL), kutokamilika mpaka sasa.
Alisema uchambuzi wa kamati yake katika ripoti ya CAG pamoja na mahojiano na uongozi wa UDSM, umebaini dosari kubwa katika usimamizi na uendeshaji wa mradi huo, hali ambayo inaipa serikali hasara.
Alizitaja dosari hizo kuwa ni pamoja na Dola 75 ambazo zilionyeshwa kama mtaji wa MHL ambao ni kinyume cha Sheria ya Uwekezaji ya Mwaka 1977 inayoelekeza kwamba, ili kibali cha uwekezaji kitolewe lazima mwekezaji awe na mtaji wa kutosha.
Mbunge huyo wa Same Mashariki (Chadema) alisema kamati yake pia imebaini Turnstar Holding Limited ni miongoni mwa wanahisa wa MHL na anamiliki hisa moja na kwamba kampuni hiyo imetoa mikopo kwa MHL jumla ya Dola za Marekani 49,027,840.
"Kamati ilipata mashaka kuhusu nia hiyo ya mbia huyu kwa kuwa MHL ana hisa 900 ambazo hazijauzwa na hivyo angenunua badala ya kukopesha. Kamati inaona mbia huyu ana lengo lake la kujinufaisha zaidi kwa kutoa mikopo kwa vile riba anayolipwa inatolewa kwenye mapato ghafi kabla ya kugawana faida," alisema.
Kaboyoka pia alibainisha kuwa kwa miaka 13 tangu mkataba huo uingiwe, mradi wa ujenzi wa hoteli ya nyota tatu yenye vyumba 100 bado haujaanza, kinyume cha makubaliano, hivyo kuongeza gharama za kumalizika kwa mradi. Pia mradi wa utengenezaji wa bustani ya wanyama na mimea (Botanical Garden) uliopaswa kwenda sawia na hoteli hiyo haujatekelezwa.
Aliongeza kuwa kumekuwapo ukiukwaji wa malipo ya pango la ardhi ya chuo ambapo vifungu cha 1.1(j) na 10.1 vya mkataba vinaeleza kuwa UDSM itapata asilimia 10 ya pango la mapato ghafi, lakini MHL imekuwa ikifanya malipo ya pango kwa chuo baada ya kutoa gharama za uendeshaji, hivyo kuikosesha serikali mapato stahiki kinyume cha mkataba.
Pia alisema wamebaini kukiukwa kwa kifungu cha 12.2(l) cha hati ya makubaliano ya mpangaji kinachomtaka MHL kutopangisha mtu yeyote ambaye hajathibitishwa na mpangishaji (UDSM).
Alisema ukaguzi wao umethibitisha kuwa MHL amekuwa akipangisha wapangaji wengine bila kupata kibali cha chuo hivyo kusababisha chuo kukosa taarifa sahihi za mapato ya kodi kutoka kwa wapangaji wake.
Kaboyoka alisema kamati hairidhishwi na mazungumzo yanayoendelea kati ya UDSM na MHL kwa kuwa mwekezaji huyo amekuwa akiyakataa mapendekezo yote yenye maslahi kwa pande zote mbili badala yake amekuwa akishikilia mapendekezo yenye maslahi kwake tu.
"Wakati huo MHL ameongeza eneo la maduka na maegesho ya magari ambayo hayakuwamo katika mkataba.
Kama hiyo haitoshi, mwekezaji ameshindwa kuanza utekelezaji wa ujenzi wa hoteli na Botanical Garden ambavyo vipo kwa mujibu wa mkataba," Kaboyoka alisema.
Kigogo wa PAC huyo alisema mapitio ya mkataba yamebainisha kuwa hauelezi hali ya ugawanaji mali pindi mkataba utakapomalizika (miaka 50 au 85) kwa kuwa hakuna makubaliano rasmi yanayoeleza mgawanyo wa mali na miundombinu itakayokuwapo pindi mkataba utakapoisha.
Alibainisha kuwa athari ya jambo hilo ni kuwa kuna uwezekano mkubwa kutokea mvutano wa kisheria pindi mkataba huo utakapofika ukomo.
Kaboyoka alisema dosari nyingine ni kuhusu ushiriki wa serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) ambapo kituo hicho na MHL wamekuwa wakibadilisha muda wa utekelezaji wa mradi mara kwa mara kwa kumwongeza mwekezaji muda wa kukamilisha mradi bila kukihusisha chuo.
"Kwa mfano, mkataba wa kwanza ulisainiwa Februari 27, 2006 na kumwongeza mwekezaji kipindi cha utekelezaji wa mradi hadi Oktoba 30, 2009. Mkataba wa pili ulisainiwa Julai 13, 2007 kwa kuongeza muda wa utekelezaji hadi Novemba 30, 2013 na mkataba wa tatu ulisainiwa Desemba 10, 2014 ambao uliongeza muda wa utekelezaji wa mradi huo hadi Desemba 31, 2019," alisema.
Kaboyoka pia alisema mkataba unaonyesha kuwa zilitakiwa kujengwa nyumba 50 za kuishi (house estate/villas) lakini kamati yake ilipotembelea mradi huo zilizonekana nyumba 45 na nyumba moja yenye vyumba viwili vilivyotenganishwa na milango miwili.
Kutokana na dosari hizo, Kaboyoka alisema mradi wa Mlimani City unapaswa uangaliwe kwa kina kuanzia mkataba wa kwanza hadi hapo ulipofika sasa.
Social Plugin