Siku 10 baada ya wanachama wa Chadema kukamatwa na polisi eneo la Mkwajuni wilayani Kinondoni jijini Dar es salaam, chama hicho kimelalamika baadhi yao kuendelea kushikiliwa na polisi katika kituo cha Oysterbay wakiwa na majeraha ya risasi bila kupatiwa matibabu, wala kufikishwa mahakamani.
Wakati chama hicho kikuu cha upinzani nchini kikieleza hayo, Polisi Mkoa wa Kinondoni wamesema hakuna mahabusu mgonjwa anayeshikiliwa bila kutibiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Murilo alisema jana kwamba, polisi wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mahabusu wagonjwa wanatibiwa katika hospitali za Serikali bila malipo yoyote.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema jana alisema wanachama wao watatu walishambuliwa kwa risasi Februari 16.
Mrema alibainisha kuwa wanachama hao walishambuliwa kwa risasi wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakielekea ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wa ubunge Jimbo la Kinondoni kudai barua za viapo vya mawakala wao.
Aliwataja wanachama hao kuwa ni Isaack Ngaga, Erick John na Aida Oromi.
“John na Ngaga wao walikamatwa wakiwa majumbani mwao baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali. Hawa hawakukamatiwa kwenye vurugu,” alisema Mrema.
“Mmoja kati yao (John) alikamatwa na watu waliojifanya watumishi wa haki za binadamu na kudai wanataka kwenda kumhoji, alipokataa ndipo walitoa vitambulisho vyao vinavyoonyesha wao ni Polisi.”
Alisema hatua iliyochukuliwa hadi sasa ni kuwaelekeza wanasheria wa Chadema kufungua kesi Mahakama Kuu kumshtaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali na polisi, kuwataka wawafikishe mahakamani wanachama hao.
“Tumemwelekeza mwanasheria wetu kufungua kesi ili wanachama wetu hao watatu wapelekwe mahakamani na kupatiwa matibabu,” alisema Mrema.
Alisema kuendelea kushikiliwa bila kupelekwa hospitali wakati wana majeraha ni hatari kwa maisha yao, kwa kuwa vidonda hivyo vitaoza.
“Wanakaa nao kinyume na sheria, mpaka sasa walipaswa wawe wameshawapeleka mahakamani,” alisema.
Kwa upande wake, Murilo alisema sheria ipo wazi inawaelekeza mahabusu wote wanapougua kutibiwa.
“Si hao mahabusu wa Chadema pekee, mahabusu yeyote anapougua hupelekwa hospitali za Serikali ambako hutibiwa bure kwa mujibu wa sheria,” alisema.
“Kama wanaolalamika wangekuwa mahabusu ningekuwa na cha kuzungumza, lakini kama wapo nje waache waendelee kusema, ninachojua hakuna mahabusu ambaye hajatibiwa.”
Mmoja wa ndugu wa Aida, Hilda Sigala alisema, “Jana (juzi) nilikwenda kumtembela ndugu yangu kituoni. Amenieleza kuwa mpaka sasa hajapelekwa hospitali na wanampaka dawa tu ya kukausha kidonda wakati ana jeraha la risasi. Yupo kituoni tangu Februari 16.”
Alisema hali hiyo si sahihi kwa sababu kidonda alichonacho Aida kinazidi kuwa kikubwa jambo ambalo ni hatari kwa afya yake.