DC NDAGALA AWAMWAGIA SIFA WANAKIJIJI RUHURU KUJITOLEA KUJENGA ZAHANATI YAO

Wananchi wa kijiji cha Ruhuru wilayani Kakonko mkoani Kigoma wamejitolea kuanza ujenzi wa zahanati itakayogharimu zaidi ya milioni 50 ili kutatua changamoto ya kutembea zaidi ya saa matatu kufuata huduma za afya hali inayosababisha wengi wao kupoteza maisha kwa kukosa huduma hiyo.

Wakizungumza jana wakati wa ziara ya mkuu wa wilaya hiyo Kanali Hosea Ndagala, kukagua ujenzi wa zahanati hiyo inayojengwa kwa nguvu za wananchi, wananchi hao waliiomba serikali kuchangia jitihada hizo walizoanzisha za kujenga msingi na kuinua ukuta ilikumaliza tatizo hilo walilonalo la ukosefu wa kituo cha afya na zahanati.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Ruhuru Bahati Kimpaye  alisema Kijiji hicho kina wakazi 2016 ambao wameamua kuanzisha ujenzi wa zahanati hiyo baada ya kuona wananchi wanapata shida ya huduma ya afya hasa wajawazito ambapo usafiri mkubwa kwao ni pikipiki kwenda umbali wa saa mawili na baadhi wanalazimika kutembea kwa miguu umbali wa saa matatu kufuata huduma katika vijiji vya Gwarama, Nyakayenzi na Nyanzige na endapo mwananchi atakosa fedha anashindwa kwenda na wengine kupoteza maisha.

Alisema hali hiyo iliwaumiza sana na kuamua kufanya mkutano wa wananchi na kukubaliana kuanzisha ujenzi huo baada ya kulifikisha halmashauri walifanyiwa tathmini na walipewa eneo ambapo gharama zilizo kadiliwa ni kiasi cha shilingi milioni 54 ambapo Wananchi walitakiwa kukusanya asilimia 20% kwa kukusanya tofali na mawe serikali iwajengee baada ya kuona wana uhitaji mkubwa wa zahanati hiyo wameamua kuanza kujenga wenyewe kabla ya serikali.

Kwa upande wake Nesia Semagogwa, mkazi wa Kijiji hicho alisema kipindi cha nyuma wanawake walikuwa wakipimiwa ujauzito kwenye gari lakini kwa kipindi hiki gari hilo halikuwa linakuja kijijini hapo hali iliyowatia uchungu kutokana na wenzao wengi kupoteza maisha na kuamua kushirikiana na viongozi wao katika ujenzi wa Zahanati ilinawao waweze kupata huduma kama vijiji vingine.

"Tunatoka hapa kwa miguu kwenda kijiji cha tatu ambacho ni Nyakayenzi yaani tunatumia muda mrefu na tunachoka sana tunaenda tunarudi jioni tunashinda na njaa yaani suala hili linatuumiza sana, tunatamani zahanati hii iishe mapema, ili iweze kutusaidia na sisi tunateseka mno jamani mtusaidie kumaliza na sisi tuepukane na adha hiii", alisema Semagogwa.

Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala aliowapongeza wananchi hao kwa kujitolea katika ujenzi huo na kuahidi kuwapatia mifuko 20 ya simenti yeye binafsi na kwamba kuna fedha kiasi cha shilingi milioni 100 zimetolewa kwaajili ya ujenzi wa vituo vya afya zitatolewa kwaajili ya kijiji hiki muweze kumalizia zahanati na kununua vifaa kutokana na changamoto waliyonayo.

"Moja ya changamoto mliyoiona ni changamoto ya zahanati niwashukuru kwa hilo na sisis kama serikali tutawaunga mkono na serikali inataka kila kijiji kiwe na Zahanati na kata kuwa na kituo cha afya mmeonesha mfano katika wilaya ya Kakonko nyie ndio watu wa kwanza kujenga zahanati wenyewe na serikali ndiyo inachokitaka hiki nyinyi mkijenga wenyewe mtasimamia ipasavyo na hamtamfumbia macho yeyote atakae jitokeza kufanya uharibifu kwakuwa mnauchungu nayo niwapongeze kwa hilo", alisema Kanali Ndagala.

Hata hivyo Kanali Ndagala amewaagiza wananchi na viongozi wa vijiji vingine kuiga juhudi hizo serikali inahitaji wananchi kuwa na umiliki wa miradi lazima waanze kwa juhudi zao na kuahidi kuwapeleka Wananchi wanaosua sua kuchangia shughuli za maendeleo kwenda kuangalia wenzao walioanza kujitolea ilikuweza kupata zahanati yao binafsi ni jambo la kuigwa na wananchi wote.

ANGALIA PICHA
Mkuu wa wilaya ya Kakonko mkoani KigomaKanali Hosea Ndagala akishiriki ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Ruhuru -Picha zote na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post