Viongozi wa Jumuia ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Kigoma Mjini wametoa mifuko 10 ya saruji na mifuko 10 ya chokaa kwa ajili ya kujenga matundu nane ya vyoo shule ya msingi Airport iliyopo Manispaa ya Kogoma Ujiji mkoani Kigoma.
Shule hiyo inakabiliwa na changamoto za upungufu wa madarasa, madawati pamoja na uhaba wa vyoo hali inayosababisha walimu na wanafunzi kuchangia vyoo na baadhi ya wanafunzi kukaa chini wakati wa masomo.
Awali akitoa taarifa kwa viongozi hao,waliotembelea shule hiyo jana, Mwalimu mkuu shule ya msingi Airport Agnes Nyamondo alisema shule hiyo ina vyumba vya madarasa nane na wanafunzi 1,644 ambapo kila darasa linachukua zaidi ya wanafunzi 250 hali inayosababisha wanafunzi kupata shida na walimu kupata changamoto katika ufundishaji.
Alisema kdarasa la pili ambalo zaidi ya wanafunzi 217 wanakaa chini kwa ajili ya kukosa madawati.
Katibu wa Umoja wa Wazazi Wilaya ya Kigoma Mjini Dorisi Kibabi, alisema siku zote uchungu wa Mwana ana ujua mzazi, katika jitihada za kuiunga mkono serikali ya awamu ya tano ya kutoa elimu bure wao kama Jumuia wameamua kuadhimisha wiki ya jumuiya hiyo kwa kutoa zawadi ya saruji 10 na mifuko ya chokaa 10 kwa ajili ya kutatua changamoto iliyopo.
Alisema baada ya kutembelea shule hiyo walipatwa na uchungu kuona watoto wanatumia vyoo pamoja na walimu wao, na vyoo visivyo na ubora hivyo wao kama umoja wa wazazi wameamua kujenga matundu nane ili kuweza kuondoa kero hiyo na watoto wasome kwa amani na kuwajengea msingi bora watoto.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kigoma Mjini, Yasini Matalikwa alisema wananchi nao wanatakiwa kuchangia kwa nafasi yao, japokuwa serikali imetoa utaratibu wa elimu bure ni lazima wananchi na wao wachangie, kwa kuwa na serikali haiwezi kufanya mambo yote peke yake lazima wananchi wajitoe na Wao katika kuchangia ili serikali iongezee mahali walipo shindwa.
Alisema suala hilo la changamoto atalifikisha kwa Waziri wa elimu iliaweze kuiingiza shule hiyo katika shule zinazo hitajika kufanyiwa marekebisho ili wanafunzi na wao waweze kupata haki yao ya msingi ya kupata elimu bora.
Akipokea msaada huo uliotolewa na umoja wa wazazi Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji John Shauri aliwapongeza na kuwaomba wananchi na wengine kuiga mfano huo kwani serikali pekee haiwezi kumaliza changamoto zilizopo katika secta ya elimu, fedha zinazotolewa ni ndogo na haziwezi kumaliza changamoto hizo.
Alisema katika shule hiyo walishatoa kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa choo lakini mpaka sasa mkandarasi huyo ameshindwa kumaliza kazi hiyo na kudai hadi aongezewe kiasi cha shilingi milioni saba na kutoa siku sita awe amefika shuleni hapo kumaliza kazi hiyo akishindwa watatafuta fundi wao na hawatamalizia kumlipa fedha zilizobaki.
Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Viongozi wa Jumuia ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Kigoma Mjini wakikabidhi mifuko ya saruji katika shule ya msingi Airport.Picha zote na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog
Mifuko ya saruji na chokaa
Social Plugin