Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MBUNGE : SITAMANI KUOLEWA WALA CHOCHOTE


MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Martha Mlata amesema tangu 2002 mpaka sasa anaishi mwenyewe na watoto wake huku akieleza kuwa hana mpango wa kuolewa baada ya kupata changamoto nyingi alipokuwa kwenye ndoa.

Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa wa kongamano lililoandaliwa na kituo cha redio EFM kwa wanawake wanaolea wenyewe 'single mothers'.

"Sitamani hata kuolewa wala chochote kwani tangu nilipoolewa mwaka 1964 nilipata watoto watatu ambao sasa ni wakubwa. Lakini nilipata mzigo mkubwa kuwaambia watoto baba yao yuko wapi, ni mzigo mzito sana," alieleza Mlata.

Mwanasiasa huyo ambaye pia ni mwimbaji wa nyimbo za injili, ametoa mwito kwa wanawake waendelee kuwa majasiri kuwaeleza watoto wao hali halisi na wasali ili watoto wajifunze upendo na kusamehe na kwamba wasikate tamaa katika maisha hayo.

Amesema, ipo haja ya kuwawezesha wanawake wanaolea watoto wao bila upande wa wazazi wa kiume ili waweze kujikwamua kiuchumi na kulea watoto wao.

Mlata na wabunge wengine wanawake wa Bunge la Tanzania, wameeleza namna wanavyolea watoto wao peke yao bila wenza wao kutokana na sababu mbalimbali na kupendekeza wanawake wa aina hiyo, wawezeshwe kiuchumi kukidhi mahitaji ya watoto wao.

Wametoa mwito kwa wanawake hao kupambana bila kukata tamaa, kwani wanao uwezo wa kutimiza ndoto za watoto wao ambao huenda wametelekezwa na wenza wao, magonjwa, vifo na kusababisha hali hiyo.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha, Catherine Magige alisema ana mtoto wa miaka 15 ambaye alimpata akiwa shule, na kwamba, alimnyonyesha kwa miezi minne na kisha kumuacha na mama yake.

Alisema bila kumtegemea mzazi mwenzie katika malezi, alihakikisha mtoto wake anakua vizuri na anafanya vizuri katika masomo yake ambapo kwa sasa amefaulu kwenda kidato cha tano.

"Nawaomba wanawake wenzangu kwani hata mimi naweza kusema ni single mother kwa kuwa nalea mtoto wangu mwenyewe. Niwasihi muwalee watoto wenu na msikubali kuwaacha na mama wa kambo," alisema Magige.

Pia alisema wafanye kazi kwa bidii, kwani wanaweza kuleta maendeleo bila wanaume. Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia alisema licha ya kwamba yeye si 'single mother' lakini anao wadogo zake wanaolea watoto wao peke yao, baada ya kufiwa na waume zao.

Alisema wanawake hao hawana sababu ya kukufuru au kukata tamaa, kwani yote ni mipango ya Mungu isipokuwa wanapaswa kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu ili wahudumie watoto wao.

"Niipongeze EFM na TVE kwa kuona changamoto mbalimbali walizonazo wanawake wanaolea watoto peke yao ili kuwasaidia mitaji ya biashara ili kuwalipia ada watoto wao," amesema Ghasia.

Aidha, alisema taasisi nyingine ziige mfano huo wa kuweka mipango madhubuti wa kusaidia kundi hilo la wanawake kwani wapo wengi na hawawezi kufikiwa wote bila jitihada mbalimbali. Mbunge Viti Maalumu mkoa wa Iringa, Ritha Kabati alieleza kuwa kongamano hilo linatoa funzo kwani wapo wanawake wa aina hiyo sehemu nyingi. Alisema kwamba atahamasisha waliopo mkoani mwake, waweze kukutana na kujadiliana namna ya kutatua changamoto zilizopo.

"Msijute kulea peke yenu bali mumtangulize Mungu kwa kila jambo, ninyi wanawake mna bahati ya kipekee sana hapa duniani. Mama asiposimama imara hata nyumba zitalegalega, jipeni moyo na kuheshimiana," aliongeza Kabati.
IMEANDIKWA NA FRANCISCA EMMANUEL

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com