Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya leo imemhukumu Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu kifungo cha miezi mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya kumkashifu Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga pia amehukumiwa kifungo kama hicho.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite ametoa hukumu hiyo leo saa tatu asubuhi. Kwa mujibu wa Hakimu Mteite, washitakiwa hao wana hatia kwa makosa waliyoshitakiwa.
Baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa washitakiwa, Peter Kibatala aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu mbadala kwa wateja wake.
Upande wa Mashitaka uliiomba Mahakama itoe adhabu kali ili liwe fundisho kwa watu wengine kwa maelezo kuwa, kauli za washitakiwa hao zimemfedhehesha Rais wa Tanzania.
Mahakama imekubaliana na upande wa mashitaka.
Sugu na Masonga walikuwa wanakabiliwa na shitaka moja la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli katika mkutano wa hadhara wa Mbunge huyo, uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge.
Januari 16, mwaka huu washitakiwa hao, walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa shitaka moja la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.