Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu raia wa Uganda, Winfred Businge kulipa faini ya Sh100 milioni au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela.
Businge (33), amelipa faini hivyo kukwepa kifungo.
Hukumu imetolewa leo Jumanne Februari 6,2018 na hakimu mkazi mkuu, Huruma Shaidi baada ya mshtakiwa kukiri kosa.
Mshtakiwa alifikishwa mahakamani akidaiwa kuingiza nchini dola 1 milioni za Marekani (Sh2.2 bilioni) bila kutoa taarifa kwa mamlaka ya forodha.
Businge anadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 11,2017 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.
Kesi hiyo ilikuwa ikiendeshwa na wakili wa Serikali mwandamizi, Awamu Mbagwa na mshtakiwa aliwakilishwa na wakili Hudson Ndusyepo.
Mshtakiwa aliposomewa shtaka kwa mara ya kwanza alikana na alikuwa nje kwa dhamana.
Kwa mara ya kwanza, Rais John Magufuli Desemba 13,2017 alizungumza kuhusu fedha hizo alipokuwa akifungua tawi la Benki ya CRDB mjini Dodoma.
NaTausi Ally, Mwananchi