MWALIMU MKUU ATUPWA JELA KWA KUOMBA RUSHWA YA ELFU 50 KWA MWANAFUNZI


MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Magu iliyoko Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Prosper Kagombolo amehukumiwa na Mahakama ya wilaya hiyo kwenda jela miaka mitatu ama kulipa faini isiyopungua laki tano kwa kosa la kuomba rushwa kwa mwanafunzi wake ili aweze kumpatia cheti chake cha kuhitimu darasa la saba.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mfawidhi wa Wilaya hiyo, Edmund Kente baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa ulalamikaji wakati walipokuwa wakieleza Mahakama mazingira ya tukio. Mshtakiwa alipelekwa jela baada ya kushindwa kulipa faini.

Mashahidi hao walieleza namna mwalimu huyo alivyomuomba mwanafunzi wake rushwa ya Sh 50,000 ili aweze kumsaidia kupata cheti chake huku akijua ni kinyume na taratibu za nchi kupitia kifungu cha sheria namba 15 (1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.

Hakimu huyo aliiambia Mahakama kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ipo katika kuwatendea haki watu wanyonge, hivyo watumishi wa serikali wasijione kuwa wako juu ya sheria kuliko watu wengine na wanaweza kuvunja sheria na wasichukuliwe hatua kwa kuogopwa kuwa ni watumishi wa serikali.

Aidha Kente aliwapongeza maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa jinsi wanavyojitaidi kupambana na watu wanaokwenda kinyume na maadili ya kazi za utumishi wa umma.

Akitoa ushahidi kwenye Mahakama hiyo ya Wilaya, Mwendesha Mashitaka wa Takukuru Maximiliani Kyabona alisema kuwa walipata taarifa za mwalimu huyo kuomba kiasi hicho cha fedha kutoka kwa mwanafunzi wake aliyemfundisha miaka ya nyuma mara baada ya mwanafunzi huyo kwenda shuleni hapo kuomba cheti chake.

“Mwalimu alimuomba kijana huyo kiasi cha Sh 50,000 kwa lengo la kutaka kumsaidia, ndipo mwanafunzi huyo (jina linahifadhiwa) alifika ofisini kwetu kuomba msaada juu ya jambo huilo,” alisema.

IMEANDIKWA NA SHUSHU JOEL- HABARILEO MAGU

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post