Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWANAMKE ACHOMWA MOTO NA WAGANGA WA JADI ILI APATE UJAUZITO



Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, linawashikilia waganga wa jadi wawili ambapo mmoja ni mkazi wa Kijiji cha Obwere na Michael Jacob wa Omuga kwa tuhuma za kumjeruhi kwa kumuunguza moto, Emiliana Thomas anayeishi Kijiji cha Omuga wilayani Rorya.


Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Henry Mwaibambe alisema jana kuwa, majeruhi huyo ambaye ni mwanamke anayesumbuliwa na tatizo la kutopata ujauzito, waganga hao walimwaminisha kuwa ataupata.


Alisema walimwambia ili apate mtoto ni mpaka kuku imwagiwe mafuta ya taa na iteketezwe moto huku mama huyo akiwa ameishikilia mikononi.


Kamanda alisema baada ya waganga hao kuwasha moto ulimunguza na kumsababishia majeraha.


Mwaibambe alisema, awali waganga hao walimweleza mwanamke huyo kuwa anasumbuliwa na mashetani ndani ya tumbo na ndio yanayomfanya asizae.


Alisema walimweleza kwamba kuku ikiteketea ikiwa mikononi mwake atakuwa ameondokana na mashetani, hivyo ni lazima iteketezwe.


Kamanda huyo alisema baada ya waganga hao ‘kumsomesha’ mwanamke huyo alikubali na ndipo walipoimwagia mafuta ya taa kuku hiyo na kuwasha moto kwa kibiriti uliolipuka na kumjeruhi kifuani na mikononi.


Mwaibambe aliongeza kuwa, hali ya mama huyo ni mbaya na anaendelea na matibabu katika Hospital ya Kowak wilayani humo.


Mmoja wa waganga hao wa jadi, Jacob alisema tukio hilo ni ‘bahati mbaya’.


“Alikuja akiomba tiba, sasa kwa bahati mbaya mafuta yalikuwa yamemumwagikia mikononi na mikono ya nguo aliyokuwa amevaa ilikuwa hadi mikononi, wakati tumewasha moto ndipo ukamuunguza,” alisema Jacob.


Akizungumza na gazeti hili, mwakilishi wa Chama cha Tiba Asili mkoani Mara, Jacob Matiko alilaani kitendo hicho kuwa hakiendani na taratibu za tiba na kinakiuka sheria inayozuia vitendo hivyo huku akiwataka waganga kutofanya utapeli iwapo hawawezi kufanya tiba kama matabibu asili.


Wakati huohuo, polisi inawashikilia watu wawili kutoka Ethiopia kwa kuingia nchini bila vibali.


Mwaibambe alisema katika tukio hilo waliwakamata pia Watanzania wawili ambao walikuwa wakiwasafirisha raia hao wa kigeni akiwamo na Pasaka Meng’anyi mkazi wa Buhemba mjini Sirari wilayani Tarime.


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Meng’anyi alieleza kuwa alipewa kazi ya kuwapokea raia hao kutoka Stendi ya Tarime hadi Mwanza na wakifika mjini humo kuna mtu atakayewapokea.


Alisema ili kufanikisha kazi hiyo alilipwa Sh300,000 huku mwenzake akiahidiwa kulipwa 100,000 ambazo bado hajalipwa baada ya kuwatoa Sirari hadi Stendi ya Tarime.
Na Dinna Maningo, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com