Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro leo amehudhuria mahafali ya pili ya chuo cha ufundi Cherehani kwa taaluma ya ushonaji nguo na ujasiriamali kwa wanafunzi wa kike 12 wenye ualbino kilichopo Mwasele Kata ya Kambarage kinachosimamiwa na Kanisa la KKKT Usharika wa Ebenezer Kanisa Kuu Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria.
Katika hotuba yake kwenye mahafali hayo yaliyofanyika leo Februari 1,2018 mkuu huyo wa wilaya ameeleza kusikitishwa na kitendo cha watu kuendelea kuamini kuwa viungo vya watu wenye ualbino vinaleta utajiri na kuwataka kuachana na imani hiyo na wajikite kwenye shughuli za kilimo ambazo zitawainua kiuchumi.
Alisema watu wenye ualbino ni binadamu kama watu wengine hivyo hawana utajiri wowote na kutekeleza mauaji kwao ama kuwakata viungo vyao huko ni kukiuka haki za binadamu kwani kinachowatofautisha na wenzao ni rangi yao tu.
Aliwataka mabinti 12 wenye ualbino ambao wamehitimu mafunzo hayo ya ushonaji nguo na ujasiriamali pale watakaporejea nyumbani wakatumie ujuzi huo kujikwamua kiuchumi na siyo tena kwenda kuishi maisha ya shida ikiwa nyenzo walizopewa zitawapatia utajiri wa maisha yao.
Aidha alizipongeza taasisi za kidini na mashirika mbalimbali kuendelea kushirikiana serikali kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, na kuahidi kuendelea kushirikiana nao, huku akitoa wito kwao pale wanapokwama kwenye majukumu yao wasisite kuomba msaada kwa viongozi wa serikali.
Katika hatua nyingine alilaani kitendo cha wazazi ama walezi kuwatelekeza watoto wenye ualbino husani wale wanaolelewa kwenye kituo cha Buhangija mjini Shinyanga na kuwataka wazazi hao warudi haraka kutembelea watoto wao kabla Serikali haijaanza utaratibu wa kuwasaka mmoja baada ya mwingine na kuwashughulikia kisheria.
Naye Askofu Msaidizi wa Kanisa la KKKT Usharika wa Ebenezer Kanisa Kuu Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria Traphaina Nkya,alisema wao wataendelea kushirikiana na serikali kutatua matatizo ndani ya jamii huku akimpongeza mkuu huyo wa wilaya kwa ukarimu wake alionao wa kuwa karibu na wananchi kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.
Kwa upande wake Mratibu wa mafunzo hayo kutoka kanisa hilo Matrida Sanga, alisema mahafali hayo ni ya pili ambapo wanafunzi hao walianza kusoma masomo hayo Oktoba 25 mwaka jana na kuhitimu leo Februari 2 mwaka huu ,wakiwa wanafunzi 12 kutoka mikoa ya Shinyanga na Simiyu.
Alitaja mafunzo ya ujasiriamali waliyojifunza kuwa ni Utengenezaji wa Sabuni za Kufulia,chooni, kusugulia vigae, msingi, mafuta ya kujipaka, maandazi ya kokoto,Donati, pamoja na ubuyu, mafunzo ambayo amedai yalikuwa yakifanyika kwa vitendo.
Nao baadhi ya mabinti hao wenye ualbino Veronica Lukas kutoka mkoani Simiyu, amelishukuru kanisa hilo kwa kuwapatia mafunzo hayo, ambayo yamewapatia ujuzi katika maisha yao na kuahidi kwenda kuuendeleza, huku akibainisha changamoto zitakazo wakabili ni uhaba wa mitaji na kuwaomba wadau wawasaidie kuwaondolea changamoto hiyo ambayo ndiyo inaweza kuwa kikwazo kwenye ujuzi huo walioupata.
Na Marco Maduhu - Malunde1 blog
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiongeza kwenye mahafaLi ya wanafunzi wenye ualbino ya ushonaji nguo na ujasiriamali.
Askofu Msaidizi wa Kanisa la KKKT Usharika wa Ebenezer Kanisa Kuu Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria Traphaina Nkya akimpongeza mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro kwa ukarimu wake wa kusikiliza kero za wananchi na kizitatua.
Wanafunzi wenye ualbino wakiwa kwenye mahafali yao.
Wahitimu wakiimba nyimbo kwenye mahafali yao ya kuhitimu elimu ya ushonaji nguo na ujasiriamali.
Wanaharakati wa kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye Ualbino akiwemo Vick Mtetema kutoka Shirika la Under the Same Sun.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiangalia chumba cha cherehani ambacho kinatumika kutoa elimu ya ujuzi ya ushonaji nguo kupitia mashine ya vyerehani.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiangalia bidhaa ambazo wametengeneza mabinti hao wenye ualbino.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiendelea kuangalia bidhaa za mabinti hao wenye ualbino walizotengeneza kwa mikono yao wenyewe.
Mkuu wa Wilaya akipokea zawadi ya baadhi ya bidhaa kutoka kwa mmoja wa mabinti hao Albino Veronica Lukasi kutoka Mkoani Simiyu bidhaa ambazo wamezitengeneza wao wenyewe
Wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo na wazazi wakiwa kwenye mahafali hayo
Wadau wa haki za binadamu wakiwa katika mahafali hayo.
Picha ya Pamoja Mkuu wa Wilaya Shinyanga Josephine Matiro wakiwa na wahitimu ,vingozi wa dini ,na wadau wa kupinga vitendi vya ukatili kwa Albino
Social Plugin