Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JINSI MWANAFUNZI CHUO CHA NIT ALIVYOUAWA KWA KUPIGWA RISASI NA POLISI...CHADEMA WAKIANADAMANA DAR


Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) kimesema aliyepigwa risasi jana Februari 16, 2018 eneo la Mkwajuni jijini Dar es Salaam na kufariki dunia ni mwanafunzi wa chuo hicho.

Chuo hicho kimemtaja mwanafunzi huyo kuwa ni Akwilina Akwiline aliyekuwa anasoma shahada ya kwanza ya ununuzi na ugavi.

Wafuasi hao wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe waliandamana kuelelea ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kinondoni, Aron Kagurumjuli kudai viapo vya mawakala wa chama hicho.

Ofisa Uhusiano wa NIT, Ngasekela David amesema wamepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mwanafunzi huyo.

"Ni kweli alikuwa mwanafunzi wetu na tumepokea kwa masikitiko taarifa hizi. Tunaendelea kufuatilia zaidi, "amesema David.

Leo Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amekiri mtu mmoja kupigwa risasi na polisi, wakati wakiwatawanya wafuasi wa Chama cha demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), walioandamana jana Februari 16, 2018.

Wafuasi hao wa CHADEMA wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe waliandamana kuelekea ofisi ya msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Kinondoni, Aron Kagurumjuli kudai viapo vya mawakala wa uchaguziwa chama hicho. 

Maandamano hayo yalianzia viwanja vya Buibui Mwananyamala ulikokuwa ukifanyika mkutano wa kampeni wa Chadema na yalipofika eneo la Mkwajuni wafuasi hao walitawanywa na polisi, huku mtu mmoja aliyekuwa kwenye basi la daladala akidaiwa kupigwa risasi na kufariki dunia.

Kamanda Mambosasa amesema kuwa watu hao waliokuwa wakiandamana, walizuia mabasi yanayotoa huduma ya usafiri wa mwendokasi, na kuanza fujo kwa kurusha mawe, hivyo polisi waliingilia kati na kuwatawanya kwa kufyatua risasi kadhaa hewani, na kati ya risasi zilizofyatuliwa, moja ilimpata mtu. 

“Walizuia mwendo kasi, wakaanza kupiga mawe kwa hiyo kati ya risasi za hewani zilizopigwa kuwatawanya kuna iliyompata (mtu),” alisema. 

Ufafanuzi huo wa Mambosasa licha ya kutoweka wazi kama mtu huyo aliyepatwa na risasi hiyo amefariki dunia ama la, umekuja huku ikidaiwa kuwa aliyepigwa risasi na kupoteza maisha ni mwanafunzi wa elimu ya juu. 

Taarifa za kifo cha mwanafunzi huyo zilianza kusambaa tangu jana, Ijumaa jioni katika mitandao ya kijamii sambamba na kuwekwa picha yake huku ikieleza kuwa amepigwa risasi wakati akiteremka katika basi la daladala. 

Mambosasa alipoulizwa kama mtu huyo ni mwanafunzi wa elimu ya juu amesema kuwa haijathibitishwa kama ni mwanafunzi na bado uchunguzi unaendelea ili kubaini ukweli wa jambo hilo.

“Haijathibitishwa hiyo, nipo kwenye pilika za uchaguzi, nadhani nitajibu hilo nitakaporejea ofisini na kupata taarifa,” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com