Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kinondoni (CHADEMA) Salum Mwalimu amedai sanduku la kupigia kura katika mtaa wa Idrisa Magomeni Jijini Dar es Salaam limeibwa huku watu wakishuhudia kitendo hicho kikifanyika na hakuna hatua zozote za kisheria zilizofanyika.
Salum Mwalimu amebainisha hayo pindi alipokuwa anazungumza mubashara kutoka katika kituo hicho baada ya kupata taarifa kutoka kwa mmoja wa wakala wake aliyempigia simu kumtaarifu kwamba kuna mtu ameiba sanduku la kupigia kura akiwa na gari na kutokomea pasipo julikana.
"Nimepigiwa simu na wakala wangu kuwa sanduku lilikuja na kuibwa lakini nikazungumza na msamamizi wa kituo hichi pamoja na Polisi ambae ni msamimizi mkuu wote walikiri kuwa sanduku limeibwa na kwa pamoja wote tulikubaliana kuwa sanduku liliibwa na mtu ambae alikuja na kulipora japo watu walikuwa wamekaa hapa hapa akatokomea nalo", amesema Salum.
Pamoja na hayo, Salum Mwalimu ameendelea kwa kusema "baada ya dakika kama 10 hivi sanduku likarudishwa. Sasa kinachonishangaza ni kwamba Polisi na Tume wanasema uchaguzi uendelee. Yaani kura zimeibwa na Polisi wapo na kuna mpaka wa vyeo vya juu kutoka katika Mkoa wa kipolisi Kinondoni"
Aidha, Mkuu wa kituo hicho alipofuatwa na muandishi kuulizwa juu ya sakata hilo alidai aruhusiwe kuongea jambo lolote kwa kuwa yeye hana mamlaka ya kuongea.
Kwa upande wake, Wakala wa CHADEMA katika kituo hicho, Msafiri Mussa amesema waliona gari aina 'Land Rover' na kushuka mtu mmoja akiwa na askari kisha akachukua sanduku hilo na kutokomea nalo.
Social Plugin