VIONGOZI 36 WA VYAMA VYA USHIRIKA MBARONI


MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa amewaweka ndani viongozi 36 wa Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) wilayani Masasi ambao ni wenyeviti na makatibu, kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za wakulima wa korosho zaidi ya Sh bilioni 2.3, ambazo ni malipo ya zao hilo kwa msimu wa ununuzi 2016/2017 na 2017/18.

Aidha, amemuweka ndani na kuagiza kuhojiwa meneja wa benki ya NMB tawi la Masasi, Aidan Msuya kwa tuhuma za kufanya muamala wa fedha za malipo ya wakulima Sh milioni 45 kwa zaidi ya mara 11 kwa siku moja.

Pia meneja huyo anatuhumiwa kuchelewesha kwa makusudi fedha za wakulima kutoka benki hiyo kwenda benki ya CRDB Sh milioni 91 ambazo benki hiyo ilitakiwa kuzipokea iwalipe wakulima.

Byakanwa alifikia hatua hiyo ya kuwaweka ndani viongozi hao kwenye Kituo cha Polisi wilayani Masasi jana, akiwa katika kikao maalumu baina ya wakulima na viongozi wa vyama hivyo, kilicholenga kupokea ripoti ya tume maalumu aliyoiunda wiki mbili zilizopita kwa ajili ya kuchunguza malalamiko ya madai ya fedha za malipo ya wakulima ambao hadi hivi sasa msimu wa korosho unamalizika bado baadhi ya wakulima hawajalipwa fedha zao.

Alisema kwamba kwa mujibu wa taarifa ya tume ya uchunguzi aliyokabidhiwa, kwa msimu wa mwaka 2016/17 wakulima zaidi ya 2,363 wanadai jumla ya fedha kwenye vyama vyao kati ya Sh bilioni 2.3 mpaka bilioni 3.2.

Alisema msimu wa mwaka 2017/18, wakulima 1,290 wanadai fedha Sh bilioni 1.5 mpaka Sh bilioni 1.8 na taarifa hiyo ilieleza kuwa kuna upotevu wa fedha za korosho za wakulima zenye thamani zaidi kati ya Sh milioni 222.7 mpaka Sh milioni 379.3 ambazo kama wakulima hao wangelipwa zingewaboreshea maisha yao.

“Naagiza Kamati yangu ya Ulinzi na Usalama fanyeni kazi mara moja ya kuwakamata hawa viongozi wote ambao wamehusika katika ubadhirifu huu wa fedha za wakulima na kinachotakiwa ni lazima warejeshe fedha hizi ndani ya siku 14 ili kila mkulima anayedai alipwe fedha zake,” amesema.

Kiongoiz huou amesema, kwa mujibu wa taarifa hiyo, NMB inatuhumiwa kuwa na fedha Sh milioni 91 ambazo ilipaswa kuzipeleka Benki ya CRDB kwa ajili ya malipo ya wakulima, lakini ilikaa nazo hivyo kusababisha kuchelewa kwa malipo ya wakulima kutoka Benki ya CRDB.

Amesema, NMB ilitoa mkopo wa Sh milioni 320 kwa Chama cha Msingi Mnavila bila ya chama hicho kuwa na makubaliano ya pamoja na benki hiyo kuhusu kuwepo kwa mkopo huo, na kwamba viongozi hao walishangazwa kuona mkopo huo kwenye akaunti ya chama chao, hivyo kuna harufu ya ubadhirifu kupitia wafanyakazi wa benki.

Aliagiza kuanzia sasa viongozi hao wachukuliwe hatua sambamba na kusitishwa kwa akaunti za vyama vyao pamoja na akaunti zao binafsi ili uchunguzi ufanyike na lengo la hayo yote ni kuhakikisha mkulima ni lazima alipwe fedha zake kutokana na viongozi hao, hata kwa kuwafilisi mali zao ili wakulima walipwe haki yao.

Mkuu wa mkoa ametoa siku 14 kwa tume hiyo kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama kufanya uhakiki wa idadi ya wakulima wanaodai ili walipwe fedha zao kulingana na madeni yao.

Pia aliagiza wakurugenzi wa halmashauri za Masasi wahakikishe wanawaondoa maofisa ushirika wa serikali wanaofanya kazi katika Chama Kikuu cha Ushirika Mtwara–Masasi (MAMCU) kwa vile maofisa hao kufanya kazi za vyama vya ushirika ni kinyume cha sheria ya ushirika na ni mgongano wa kimaslahi.

Akitoa mapendekezo ya tume hiyo mbele ya mkuu wa mkoa huyo wakati alipokuwa akihitimisha kusoma taarifa hiyo, Mwenyekiti wa tume, Remetus Mwabilaki alisema wanapendekeza kuwa viongozi wote waliosababisha ubadhirifu huo wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Wilaya ya Masasi ina jumla ya vyama vya ushirika vya msingi 50, ambavyo kati ya hivyo, 42 vipo katika Halmashauri ya Masasi Vijijini na nane vipo katika Halmashauri ya Mji Masasi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post