Idadi ya wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu ya mimba katika shule za msingi na sekondari nchini, imeongezeka kutoka takribani 3,000 ya mwaka 2013 hadi wanafunzi 5,033 katika mwaka 2016.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kupiga vita mimba za utotoni na rushwa mkoani Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya Watoto katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Margaret Mussai alisema ongezeko hilo linatishia maendeleo ya elimu nchini.
“Wanafunzi wengi walioacha masomo ni wa sekondari ambao ni zaidi ya 4,033 wakati wanaobaki 600 ni wa shule za msingi nchini," amesema.
Mussai alisema kutokana na kuongezeka kwa wimbi la kuacha masomo sababu ya mimba, Desemba mwaka juzi mjini Tarime, mkoani Mara, Wizara hiyo ilizindua Mpango Mkakati wa Kitaifa wa kuendesha kampeni nchi nzima kukomesha vitendo hivyo.
"Kampeni hii ni ya miaka mitano itamalizika mwaka 2019, lakini Serikali itafanya tathmini na kupima matokeo mwaka 2022, ili kuona kama tatizo limepungua au kama bado linaongezeka hatua gani za makusudi zichukuliwe kukomesha," alisema.
Katika utafiti uliofanywa na wizara hiyo, Mussai alisema imebaini kwamba watoto wengi wanapata mimba wakiwa shuleni kutokana na umasikini na umbali kutoka nyumbani hadi shuleni unaowafanya waendeshaji bodaboda, bajaji na daladala kuutumia kama mwanya wa kuwahadaa watoto kwa kuwapa lifti na hatimaye kuwaingiza katika mapenzi.
Alisema pia baadhi ya wanafunzi wanapata mimba kutokana na ukatili unaofanywa nyumbani na ndugu, jamaa na marafiki unaofikia takriban asilimia 60, huku asilimia 40 zinazobaki, watoto wakifanyiwa ukatili shuleni na baadhi ya walimu na viongozi wengine.
Mussai alisema kitaifa, wasichana 27 kati ya 100 wanapata mimba wakiwa na umri chini ya miaka 18, kitendo ambacho ni hasara kwa taifa.
Aliwataka wazazi, walimu, viongozi wengine katika maeneo yao, warudi kwenye maadili, wawalee watoto na kuwaonya athari za mimba wakiwa shuleni kwani zinafupisha na kukatisha ndoto zao za baadaye.
Akizindua kampeni ya kupiga vita mimba za utotoni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo alisema ni wajibu kwa kila kiongozi wa halmashauri kuhakikisha anasimamia kampeni hiyo na kuwataka viongozi wengine kusaidia na kuwawezesha maofisa maendeleo katika kampeni yao ya kutoa elimu kwa umma na wanafunzi.
IMEANDIKWA NA MAGNUS MAHENGE, DODOMA