ASKOFU CHENGULA: CHAGUENI VIONGOZI WASIO NA UBINAFSI NA AMBAO WATAWAFANYA MSIISHI KWA KUOGOPA OGOPA

Wakristo kote nchini wametakiwa kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2019 wa madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa na viongozi wa vitongoji kwa kumchagua mtu asiyewafanya waishi kwa kuogopaogopa.


Kauli hiyo imetolewa jana Machi 30 na Mhashamu Askofu Evarist Chengula alipokuwa akiongoza ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika kitaifa katika kanisa Katoliki la Bikira Maria wa Fatma lililopo Mwanjelwa mjini Mbeya.


Akihutubia katika ibada hiyo Mhashamu Chengula alisema ujumbe uliotolewa na maaskofu siku kadhaa zilizopita ulikuwa haumlengi mtu fulani bali uliwalenga wanafiki wanaodai ni Wakristo lakini hawana imani ya Kikristo ili waweze kubadilika na kuwa watu wema.


“Ujumbe wa mwaka huu tunasema hakuna maana kusikiliza kila kitu tu, badala yake tufikiri kabla ya kutenda.


“Imekuwa kawaida kila baada ya kumalizika uchaguzi mkuu tunaanza kulaumiana, Wakristo wote katika jumuiya zenu ndogo ndogo nchi nzima muanze kujipanga mnataka mtu wa aina gani, angalieni ana tabia gani na si anatoka chama fulani,” alisema Mhashamu Chengula. Amewataka wanaparokia kukaa na maaskofu na kujadili.


“Msipofanya hivyo mtarudi kule kule kwa kulaumiana. Chagueni kwa kuzingatia kila mmoja atendewe haki, apate haki na amani.”Alisema na kuongeza;


“Kila baada ya uchaguzi wanakimbizana kama sungura na mbwa maana hatuchagui anayetusaidia sisi, tunachagua chama fulani kituongoze na kitutetee badala ya kufikiri kuchagua atakayetuongoza kwa amani.”


Aliongoza: “Haina maana kutuchagulia watu fulani ambao tukiwachagua wanatuongoza kwa woga, hawa hawajajiweka wenyewe ni mimi na wewe tumewaweka, tusichague watu wenye roho ya ubinafsi.”


Alisema ujumbe huo ni kwa wote, ili waanze kujiandaa kwa sababu unafika uchaguzi wa mwaka 2019 wachague kwa kuangalia hali halisi.


“Kila mmoja akasimulie hili anapokwenda kwa sababu ni vita ya wote, kila mmoja awe makini Tanzania iwe na upendo na mshikamano kati yetu.


“Kila anayekuja kubusu msalaba huu tulioulaza hapo mbele amueleze Yesu nataka Tanzania yenye upendo,” alisema Mhashamu Askofu Chengula.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post