Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Tabora imemhukumu mkazi wa Manispaa ya Tabora, Sadick Masunzu (47) kifungo cha miaka minne jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka binti yake mwenye umri wa miaka 16 na kumpatia ujauzito.
Akitoa hukumu hiyo jana, hakimu wa mahakama hiyo, Joctan Rushela alisema ameridhika na maelezo yaliyotolewa na upande wa mashtaka uliokuwa ukiongozwa na wakili Tito Mwakalinga kuthibitisha bila shaka kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.
Hakimu huyo aliongeza kuwa kitendo kilichofanywa na mshtakiwa si cha kiungwana katika jamii ya Watanzania, hivyo mahakama inamtia hatiani kwa kosa hilo na inamhukumu kwenda jela miaka minne ili liwe funzo kwake na kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
Awali wakili wa Serikali, Mwakalinga alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alimbaka mtoto wake wa kumzaa na kumsababishia ujauzito.
Mwakalinga alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo katika tarehe tofauti Januari 2017 na kumsababishia ujauzito binti huyo aliyekuwa mwanafunzi wa Sekondari ya Lwanzali iliyopo katika Manispaa ya Tabora ashindwe kuendelea na masomo.
Upande wa mashtaka uliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa kwa kuwa kitendo cha kumbaka na kumtia mimba mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi kimemharibia maisha yake. Akizungumza mjini Dodoma Juni 16, 2017 katika kongamano la maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, aliyekuwa naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangalla alisema mtoto mmoja wa kike kati ya watatu anakumbana na ukatili wa kingono kabla ya kufikia umri wa miaka 18.
“Kwa mujibu wa Takwimu za Elimu kwa Mwaka 2012 hadi 2016 idadi ya watoto wa kike walioacha shule kutokana na kupata ujauzito ni 610 (mwaka 2011), 2,433 (mwaka 2012), 247 (mwaka 2013), 265 (mwaka 2014 na 251 (mwaka 2015). Serikali inaendelea kukabiliana na changamoto hizi ili kuhakikisha wanafunzi wa kike wanapata elimu hadi kufikia ngazi ya vyuo,” alisema Dk Kigwangalla.
Na Robert Kakwesi, Mwananchi
Social Plugin