MKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz, amewaita wananchi waliopotelewa na ndugu zao kufika kwa ajili ya utambuzi wa miili ya watu waliookotwa kwenye viroba pembezoni mwa bahari.
Boaz amesema tangu Jeshi la Polisi litangaze kwa wananchi kwa kuwataka waliopotelewa na ndugu kufika kutambua ndugu zao, hakuna mtu yeyote aliyejitokeza.
Oktoba 5, mwaka jana Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, alitoa wito kuwa kama kuna mtu ambaye ndugu yake amepotea afike makao makuu ya jeshi hilo kitengo cha DCI, ili kufanya uchunguzi kuona kama ni ndugu yake au la.
Pia aliwataka wananchi waliopotelewa na ndugu zao wafike kwa ajili ya kuchukua vinasaba (DNA), baada ya miili 15 kuokotwa ikiwa imefungwa kamba katika fukwe za Bahari ya Hindi.
Akizungumza na Nipashe, Boaz alisema tangu kutolewa kwa tangazo hilo hadi sasa hakuna mwananchi yeyote aliyejitokeza.
“Tangu siku hiyo mpaka sasa hatujawahi kuona ndugu hata mmoja aliyekuja kuulizia ndugu yake, Watanzania waendelee kujitokeza, na tutawatest kwa kuangalia DNA,” alisema Boaz.
Alisema kwa mwananchi yeyote atakayejitokeza atachukuliwa sampuli ya vinasaba na kuvihusisha na mwili ili kubaini kama ni ndugu yake au la.
Alipoulizwa endapo Jeshi la Polisi limeshabaini miili hiyo imetokea wapi, Boaz alisema haijajulika, na ndiyo maana walitangaza kwa yeyote aliyepotelewa na ndugu yake ajitokeze.
“Jeshi la Polisi litachukua sampuli ya DNA tutazihusisha na ndugu yake, Lazima tujue DNA hii inafanana na DNA hii,” alisema Boaz.
Alifafanua kuwa kweye utambuzi wa miili ya watu waliokufa ni lazima kiwapo kitu cha kulinganisha au kuoanisha.
Social Plugin