Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAALIMU SEIF AMLIPUA LIPUMBA "NITABAKI KUWA KATIBU WA CUF..SIFUKUZIKI"

Mgogoro wa uongozi ndani ya CUF unaendelea kukitikisa chama hicho baada ya jana katibu mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad kusema Profesa Ibrahim Lipumba hana uwezo wa kumfukuza uanachama huku akimwambia, “Sifukuziki.”


Maalim Seif alitoa kauli hiyo jana katika kongamano la kujadili mwenendo wa CUF lililofanyika Tandale jijini Dar es Salaam, kumjibu Profesa Lipumba ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.


Kauli ya makamu huyo kwa kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) mwaka 2010 hadi 2015, imekuja siku mbili baada ya Profesa Lipumba kusema Maalim Seif atajadiliwa na kamati ya maadili na nidhamu ya chama hicho kwa utovu wa nidhamu na kudhoofisha CUF.


Katika kile kilichoonekana kumjibu Profesa Lipumba, katibu mkuu huyo alisema kamwe hatakwenda kuhojiwa kwenye kamati hiyo aliyodai ni haramu akisema ipo kinyume cha sheria na taratibu za chama hicho.


“Nitabaki kuwa katibu wa chama hiki hadi uchaguzi wa CUF utakapofanyika mwakani. Kamati ya maadili inamwita Seif, Seif yupi? Siwezi kuungana na wasaliti hata siku moja na wasijisumbue,” alisema.


Alidai kwamba kuna mipango inaratibiwa ya kumfukuza katika wadhifa wake ili nafasi hiyo apewe kiongozi mmoja wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).


“Kiongozi huyo akiwa katibu mkuu, atapata fursa ya kugombea urais wa Zanzibar lakini ninawaeleza kamwe hawawezi kufanikiwa,” alisema Maalim Seif.


Akijibu madai hayo, mkurugenzi wa habari na mawasiliano kwa umma (CUF Lipumba), Abdul Kambaya alisema anachokifanya katibu mkuu huyo ni sawa na kupiga ramli akisema kitendo chake cha kutofika ofisi za chama hicho, sawa na kujifukuza.


“Maalim Seif alishajifukuzisha CUF kwa sababu hafiki ofisini Buguruni. Kwa hiyo hatuwezi kufukuzana na kulumbana na kivuli chetu wenyewe,” alisema.


Katika kongamano hilo, Maalim Seif pia aligusia jinsi Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulivyompokea aliyekuwa mgombea urais wa Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Edward Lowassa na kubainisha kuwa Profesa Lipumba alishiriki kumleta, jambo ambalo mara kadhaa msomi huyo amekuwa akilikanusha.


Pia, Maalim Seif alisema hivi karibuni atafanya ziara kisiwani Pemba na kusema anataka kujihakikishia kama kweli Profesa Lipumba ana wafuasi wengi kisiwani humo kama alivyodai baada ya ziara yake mwezi uliopita.


“Ninawataka wanachama wa CUF kuendelea na mshikamano maana haki itapatikana. Mjitokeze kwa wingi katika kesi zinazoendelea mahakamani. Tuamini kuwa haki itatendeka,” alisema Maalim Seif.


Kongamano hilo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CUF (upande wa Maalim Seif), akiwemo mkurugenzi wa uchaguzi, Sheweji Mketo na naibu katibu mkuu, Joran Bashange na madiwani.


Katika kikao cha baraza la uongozi kilichofanyika Machi 22, Profesa Lipumba alidai kuwa Maalim Seif ameidhoofisha CUF kwa kuwakumbatia viongozi wa Chadema na kutotekeleza azimio la Baraza Kuu la kufungua kesi Mahakama Kuu ya Zanzibar kupinga kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa wawakilishi na madiwani ambao alisema walikabidhiwa hati za ushindi wa majimbo na Shehia zao katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com