Mratibu wa Mashindano ya Magari Tanzania,Faheem Ao akizungumza na wandishi wa habari kuhusiana na Mashindano hayo wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mbio za Magari
Mwenyekiti wa Chama cha Mbio za Magari Mkoani Tanga Akida Machai kulia akizungumza kuhusiana na mashindano hayo
Meneja wa Mkwabi Super Market ambao ndiyo wadhamini wa Mashindano hayo,Lawi Sozigwa
***
ZAIDI ya magari 12 yanatarajiwa kushiriki kwenye michuano ya Mbio za Magari ya Mkwabi Tanga Rally 2018 yatakayoanza leo Jumamosi na Jumapili kwenye eneo la Super Market ya
Mkwabi Jijini Tanga kuzunguka maeneo mbalimbali mkoani hapa na kurejea yalipoanzia.
Hayo yalibainishwa leo na Mwenyekiti wa Chama cha Mbio za Magari Mkoani Tanga (TMSC) Akida Machai wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu kuelekea mashindano hayo.
Alisema maandalizi ya mashindano hayo hivi sasa yanaendelea vizuri ikiwemo kufanya mazungumzo na Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama Barabarani,Jeshi la Zimamoto na Madaktari kwenye hospitali ya mkoa wa Tanga Bombo.
“Kwa kweli haya ndio mashindano ya kwanza tokea mwaka huu ulipoanza hivyo tutahakikisha yanafanyika kwa mafanikio makubwa kwa lengo la kutoa burudani kwa wakazi wa maeneo yatakapokuwa yakipita kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ",alisema.
Kwa upande wake,Mratibu wa Mashindano ya Magari Tanzania,Faheem Alo alisema msimu huu mashindano hayo yatakuwa ya aina yake kutokana na kufanya maandalizi mapema jambo ambalo limeongeza hamasa.
Alisema mashindano hayo yataanza saa mbili asubuhi eneo la Mkwabi Super Market kuelekea eneo la Pongwe km 15 toka Tanga mjini na baadae kuelekea kwenye maeneo waliopangiwa kwa ajili ya kupita hivyo kuwataka wakazi wa Jiji hilo kuona namna ya kujitokeza kwa wingi kuweza kushuhudia namna
madereva wanavyochuana.
Aidha alisema kwa siku ya Jumapili mashindano hayo yataanzia Hotel ya Tanga Beach kuelekea Mkinga na baadae kwenda Duga Sigaya ambapo kwenye maeneo ambayo yatapita wananchi wametakiwa kuwa makini na watoto wao.
“Tumejipanga vizuri kwenye masuala ya ulinzi na usalama kwa kuzungumza na askari wa usalama barabarani wakiwemo wa Jeshi la Zimamoto kwa lengo la kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa mashindano hayo".alisema.
Hata hivyo aliwataka watu kuhakikisha wanazuia familia zao
zisijitokeze barabarani wakati mashindano hayo yanaendelea kwa lengo la kuepukana na madhara wanayoweza kukumbana nayo.
Naye kwa upande wake,Meneja wa Mkwabi Super Market ambao ndio wadhamini wa Mashindano hayo,Lawi Sozigwa alisema kampuni hiyo imelenga kuhakikisha mchezo huo unapata mafanikio makubwa na ndio maana wakaona watoe mchango wao huo.
Alisema pia watatumia mashindano hayo kuweza kujitangaza kwa jamii ya wakazi wa mkoa wa Tanga na nje ya mkoa kwa lengo la kuweza kutambulika zaidi.
“Sisi kama Mkwabi Super Market tumekuwa wafadhili wa mashindano hayo na sasa ni mwaka wa pili huu hivyo nisema tu tunatumia nafasi hii pia kuweza kujitangaza",alisema Sozigwa.
(Habari kwa hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha)