Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MALUMBANO YATAWALA MAHAKAMANI VIGOGO WA CHADEMA KUPEWA DHAMANA

Baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwapa dhamana viongozi sita wa Chadema, akiwamo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, malumbano ya kisheria yanaendelea mahakamani hapo.


Washtakiwa hao wametakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao watasaini hati ya dhamana ya Sh20 milioni na kuwa na barua kutoka kwa viongozi wao ama wa vijiji au mtaa, ambao watapaswa kuwa na nakala za vitambulisho vyao.


Pia, wametakiwa kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam.


Hakimu mkazi mkuu, Wilbard Mashauri amesema asiyeridhika na uamuzi huo ana haki ya kukata rufaa.


Kesi hiyo inaendelea mahakamani hapo muda huu saa tisa alasiri Machi 29, 2018 na upande wa mashtaka unaonyesha nia ya kukata rufaa.


Mmoja wa mawakili wa viongozi wa Chadema, Peter Kibatala anaipinga taarifa ya rufaa iliyotolewa na wakili wa Serikali.


Kibatala amesema mahakama itekeleze amri yake ya dhamana kwa kuwasainisha washtakiwa bondi ya Sh20 milioni katika tarehe ambayo inaona inafaa, baada ya hapo ndiyo ipokee taarifa hiyo ya Serikali ya kukata rufaa.


Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi amedai kuwa hilo ni suala la kisheria kwa kuwa taarifa ya rufaa ikishawasilishwa mahakamani na kupokelewa, mahakama husika itakuwa imefungwa mikono kuongea chochote kuhusiana na taarifa hiyo, kwa maelezo kuwa itakuwa imeingia katika kumbukumbu za mahakama.










Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com