Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameibua tuhuma nyingine mpya dhidi ya taasisi za Serikali ikiwamo polisi akidai kuwa kuna mkakati wa kuwafungulia kesi ya mauaji na uhaini baadhi ya viongozi wa chama chake.
Amedai kuwa lengo la kutekeleza mambo hayo ni kuhakikisha kuwa viongozi hao wanawekwa mahabusu kwa muda mrefu ili kufifisha na kuua upinzani nchini.
“Njama hizi zinaweza kuua baadhi, kujeruhi na hata kupoteza kadhaa lakini kamwe hazitazima njozi za kupigania haki na ustawi katika nchi yao,” amesema Mbowe katika waraka wake alioutoa jana asubuhi.
Hata hivyo, polisi imemkosoa mwenyekiti huyo kwa hatua yake ya kutoa malalamiko katika mitandao ya kijamii na kufananisha kitendo hicho na ushamba.
Mbowe alitoa waraka huo mfupi kabla ya kuwaongoza viongozi wa chama hicho kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam kuhojiwa kwa madai ya kufanya maandamano kinyume cha sheria.
Mbali na Mbowe, viongozi walioripoti polisi jana ni katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, manaibu katibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar) na mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, John Heche.
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee na mweka hazina wa baraza hilo, Esther Matiko ambao pia ni wabunge hawakuripoti polisi.
Februari 20, Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam iliagiza kukamatwa viongozi saba waandamizi wa Chadema, siku chache baada ya tukio la kuuawa kwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.
Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi Februari 16 akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakienda ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao.
Waraka wa Mbowe umetoka baada ya takribani siku 25 tangu alipozungumza na wanahabari saa chache kabla ya kuripoti polisi na viongozi wenzake.
Waraka wa Mbowe
Katika waraka huo wa jana, Mbowe anadai kuwa anazo taarifa za mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa kuunganishwa katika kesi inayowakabili.
Anadai kwamba baada ya chaguzi za Kinondoni na Siha, wamekuwa wakifuatiliwa na kwamba baada ya kuanza kuripoti polisi, njama hizo zimeendelea kupangwa na kwamba lengo ni kujaribu kuhusisha uongozi, wanachama na wafuasi wa Chadema na tuhuma za ama ugaidi, mauaji, au hata uhujumu uchumi.
“Mkakati huu unashinikizwa na viongozi wa Serikali na kuratibiwa na wasaidizi wao... Wanadhani kufanya hivyo kutamaliza vuguvugu la mabadiliko na uhitaji wa demokrasia nchini.
“Naamini kwa kuzima uongozi wa Chadema uliopo leo, sio tu kutaruhusu kuchipua kwa kasi kwa uongozi mbadala, bali pia kutaamsha ari ya Taifa kuongeza juhudi katika harakati.”
Anadai pia kwamba sasa nchi ina msiba kwa kuwa wanasiasa, wanaharakati, wanahabari na hata wasanii wanateswa, kufungwa na wengine kuuawa. “Wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na nje wanalia. Viongozi wa dini wanachanganyikiwa. Wakulima, wafugaji na wavuvi wako hoi, hata watoto na wanafunzi nao ni tishio kwa watawala. Wengi wanataabika wanaisubiri fursa iwavyo vyovyote vile.”
Mnyika, Heche wabanwa polisi
Baada ya Mbowe na viongozi hao kuripoti polisi na kukaa kituo hapo kwa takribani saa tatu, waliachiwa huku Mnyika na Heche wakibaki na kuhojiwa kwa zaidi ya saa 2:30 kutokana na kutoripoti kituoni Machi 16.
Mara baada ya kuachiwa na kutakiwa kuripoti Machi 27, Heche ambaye pia ni mbunge wa Tarime Vijijini alisema kitendo cha viongozi wa Chadema kuripoti polisi na kukaa kwa saa tano bila kuhojiwa chochote na kutakiwa kuripoti siku nyingine ni sawa na kifungo cha nje.
“Hii ni mara ya tano ninaripoti polisi. Polisi Tanzania ni kama wametuhukumu kifungo cha nje, kila baada ya siku mbili wanataka turipoti Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam bila kujali unaishi wapi, gharama unazotumia kuja na kurudi Dar es Salaam na majukumu yako mengine ya kikazi unayoshindwa kuyatekeleza,” alisema.
Wakili wa viongozi hao, Frederick Kihwelo alisema Mnyika na Heche walizuiwa kuondoka na kutakiwa kuandika maelezo.
“Baada ya kufika, polisi waliwataka Heche na Mnyika ambao hawakufika Machi 16 wabaki baada ya wenzao kuondoka na kuwaagiza kuandika ahadi ya maandishi kuwa Jumanne ijayo watakuwepo,” alisema.
Hata hivyo, polisi walikanusha madai ya Kihwelo kuwa wanataka kuwakamata Mdee na Matiko popote walipo.
Na Tausi Mbowe na Fortune Francis, Mwananchi
Social Plugin