Mabula Mabula amekiri mbele ya jeshi la polisi na waandishi wa habari kufanya matukio mbalimbali ya ubakaji, uporaji na kujifanya polisi.
Akihojiwa mara baada ya kutiwa mbaroni na jeshi hilo, Mabula maarufu kwa jina la Six alieleza kinagaubaga namna alivyofanya uhalifu huo ikiwa ni pamoja na kuwatishia mapanga wanawake, kuwabaka na kuwapiga picha za utupu na baadaye kutishia kuzituma kwenye mitandao ya kijamii.
“Hizo picha huwa nawapiga kwa kutumia simu zao na anayekataa kunipa hela huwa naondoka na simu yake na kisha natuma hizo picha kwenye mitandao iliyopo kwenye simu hizo, baada ya hapo simu naiuza napata hela,” alisema Six.
Mabula alieleza mbinu nyingine anazotumia kuwa ni pamoja na kujifanya ofisa wa polisi na kisha kuwakamata wanawake hao na kuwasingizia makosa mbalimbali kabla ya kuwabaka.
Mtuhumiwa huyo aliyataja maeneo anayofanyia matendo hayo kuwa ni Msamvu Relini na kwamba amekuwa akitumia mapanga kuwatisha wanawake na kuwapiga picha za utupu na baadaye kutishia kuzituma picha hizo kwenye mitandao ya kijamii.
Akizungumzia tukio hilo jana, kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Mtei alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya mwanamke mmoja kutoa taarifa za malalamiko ya kufanyiwa vitendo hivyo.
“Makachero na askari wa kikosi cha kupambana na uhalifu wa mitandaoni na kikosi cha kupambana na ujambazi walianza kumfuatilia kwa ukaribu na kufanikiwa kumkamata baada ya kupata taarifa kutoka kwa mwathirika,”alisema kamanda huyo.
Katika mahojiano na polisi, mtuhumiwa huyo alimtaja mwezake mmoja (jina tunalo) maarufu kama ‘miondoko’ mkazi wa Manispaa ya Morogoro kuwa ndiye mnunuzi wa simu hizo za wizi.
Katika msako huo polisi walimkamata rafiki huyo wa Mabula na kwamba wote watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Tukio linalofanana na hilo ni lile lililotokea Morogoro mwaka 2016. Katika tukio hilo la miaka miwili iliyopita wanaume wawili walimlazimisha mwanamke kufanya mapenzi na kisha kumrekodi picha za video na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa Kamanda Matei, wanaume hao walimtishia kisu msichana huyo asipige kelele wakati akifanyiwa kitendo hicho.
Katika tukio jingine polisi wanamshikilia Maulid Mohamed, Saimon Donard na Aginiwe Naftari wote wakazi wa Manispaa ya Morogoro kwa tuhuma za utapeli kwa njia ya mitandao.
Kamanda Matei alisema watuhumiwa hao walikamatwa Machi 20 baada ya kumtapeli mtu mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa kiasi cha Sh115, 000 kwa madai kuwa wana biashara ya vinyago.
Alisema matapeli hao walimrubuni kuwa kiasi hicho cha pesa ni kwa ajili ya kusafirisha vinyago hivyo mpaka jijini Dar es Salaam na baadaye wangegawana faida.
Watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na simu tisa za aina mbalimbali, kitambulisho cha kupigia kura, laini 57 za mitandao mbalimbali na karatasi sita za kitabu cha kumbukumbu za wakala wa mtandao (log book) mmoja wa simu ambao umehifadhiwa.
Na Hamida Shariff, Mwananchi
Social Plugin