MWANAFUNZI WA KITANZANIA AFARIKI KWA KUGONGWA GARI NA WASIOJULIKANA AFRIKA KUSINI


Mwanafunzi wa Kitanzania aliyekuwa akisoma Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Johannesburg (UJ), Afrika Kusini, Baraka Nafari amefariki dunia kwa kugongwa na gari na watu wasiojulikana akitokea katika matembezi ya usiku.


Uwezo Edward, ambaye ni binamu wa Baraka anayeishi Afrika Kusini amesema hana uhakika iwapo ndugu yake alikuwa na adui au ugomvi na mtu, lakini mazingira ya kifo chake yana utata.

Akizungumza na MCL Digital leo Machi 2, 2018, Edward amesema Baraka ataagwa Jumanne wiki ijayo na baada ya hapo wataanza safari ya kuuleta mwili nchini.

“Alhamisi ya wiki ijayo tutausafirisha mwili wa mpendwa wetu kuelekea mkoani Kigoma kwa ajili ya kuupumzisha kwenye makazi ya milele,” amesema Edward.

Akizungumzia suala hilo, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Augustine Mahiga amesema bado ofisi yake haijapata taarifa yoyote kuhusiana na suala hilo.

Amesema yupo nje ya ofisi lakini kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji hadi asubuhi hakukuwa na taarifa kutoka Ubalozi wa Afrika Kusini kuhusu kijana wa Kitanzania kufikwa na umauti.

“Ngoja niwasiliane na wenzangu waliopo ofisini muda huu wawasiliane na ubalozi wetu nchini humo kwa maelezo zaidi, kama limetokea pia lazima wakusanye taarifa za kina kabla ya kuzituma, hilo linaweza kuchelewesha kutufikishia taarifa mapema,” amesema Balozi Mahiga.

Chanzo- Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post