Mwanamke aliyeangua kilio mbele ya Rais John Magufuli wakati wa maadhimisho ya siku ya sheria jijini Dar es Salaam, Februari 2, mwaka jana, amehukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela baada ya kukutwa na hatia ya kuingia sehemu isiyoruhusiwa bila kibali.
Swabaha Shosi, ambaye baada ya tukio hilo alizua mjadala mkubwa, jana haikuwa siku njema kwake kwani alijikuta akiangukia mikononi mwa sheria baada ya Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Usambara, Khadija Kitogo kumtia hatiani kwa kuingia eneo lisiloruhusiwa kisheria.
Swabaha alifikishwa mahakamani hapo Agosti 9, mwaka jana akitakiwa kujibu shtaka la kuingia katika eneo la Chongoleani ambako hakuruhusiwi raia kuingia.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa aliingia katika eneo lililokuwa limetengwa kwa ajili ya ujio wa marais, John Magufuli na Yoweri Museveni wa Uganda walipokwenda kuzindua mradi wa bomba la mafutaghafi kutoka Uganda hadi Hoima, Agosti 5 mwaka jana.
Upande wa utetezi ulikuwa na mashahidi wawili, Swabaha mwenyewe na mtu mwingine huku upande wa mashtaka ukiwa na mashahidi wawili ambao ni maofisa wa polisi waliokuwepo eneo la Chongoleani siku ya tukio.
Hata hivyo, Swabaha alikana mashtaka hayo akijitetea kuwa alikanyaga eneo hilo wakati akiandaa eneo kwa ajili ya kuwauzia chakula waliohudhuria uzinduzi huo na kwamba hakuwa peke yake, bali walikuwapo watu wengine.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Kitogo alisema baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, mahakama imemkuta na hatia ya kuvunja Sheria ya Makosa ya Jinai, kifungu namba 299 sura ya 19.
“Ninampa adhabu ya kwenda jela miezi mitatu ili iwe fundisho kwa wengine wanaovunja sheria kwa kuingia maeneo yasiyoruhusiwa,” alisema Hakimu Kitogo.
Mwanasheria wa mjane huyo, Shukuru Khalifa alisema atawasilisha maombi ya kukata rufaa mahakamani. “Nitapeleka maombi ya rufaa ili wakati rufaa ikisikilizwa, mteja wangu awe nje kwa dhamana,” alisema Khalifa.
Alisema hukumu hiyo ina upungufu kisheria kwa sababu hakukuwa na chaguo la kulipa faini, jela au kifungo cha nje kutokana na uzito wa kosa lenyewe.
Swahaba alipata umaarufu nchini baada ya kuwasilisha kilio chake mbele ya Magufuli wakati wa maadhimisho ya kilele cha Siku ya Sheria Februari 2, mwaka jana.
Baada ya Rais Magufuli kuhutubia siku hiyo, mama huyo alisimama na bango lake la kitambaa lililokuwa na ujumbe uliokuwa ukimlalamikia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na polisi kuwa wanashirikiana na mwanasheria na watu wengine kumdhulumu haki yake ya mirathi.
Alimwambia Rais kuwa amedhulumiwa mirathi ya mumewe Mohammed Shosi Yusufu na alidai kuna wakili aliyetengeneza wasia wa kughushi huku akiwatuhumu polisi na DPP kuwa wanashirikiana kumlinda.
Katika kesi hiyo ya mirathi, Swabaha alimfungulia mashtaka Saburia Shosi, ambaye ni mtoto wa marehemu Shosi aliyeteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu baba yake.
Hata hivyo, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Amour Hamis, alitoa uamuzi akisema mahakama hiyo imeridhika na hukumu iliyotolewa awali na mahakama ya wilaya na ile ya mwanzo ya kumfanya Saburia kuwa msimamizi wa mirathi.
Na Burhani Yakub, Mwananchi
Social Plugin