Jeshi la Polisi mkoani Mara linaendelea na msako dhidi ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya mfanyabiashara na mmiliki wa kampuni ya mabasi ya Super Sami, Josia Mzuri maarufu kwa jina la Samson ambaye mwili wake ulikutwa kwenye viroba ndani ya Mto Ndabaka mpakani mwa wilaya za Bunda na Busega.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, kamanda wa polisi Mkoa wa Mara, Jaffari Mohamed alisema pamoja na msako dhidi ya watuhumiwa wengine, pia jeshi hilo linaendelea kuwahoji watu wanne wanaoshikiliwa kuhusiana na tukio hilo.
Kamanda Mohamed alitoa wito kwa watu wenye taarifa zitakazosaidia kuwanasa wahusika au kufanikisha ushahidi dhidi ya watuhumiwa wanaoshikiliwa kujitokeza kuziwasilisha polisi.
“Suala hili linahitaji uchunguzi wa kina si tu kubaini na kuwanasa wahusika, bali pia kupata ushahidi wa kina unaotosheleza kuwatia hatiani. Tunaomba raia wema washirikiane na polisi kukamilisha jukumu hilo,” alisema.
Kauli ya kamanda huyo inakuja baada ya zaidi ya wiki moja tangu mwili wa Mzuri ukutwe mtoni na kuzikwa nyumbani kwake mtaa wa Majengo ya Chini mjini Magu mkoani Mwanza.
Baadhi ya wafanyabiashara wenzake na Josia walielezea kuingiwa na hofu juu ya usalama wao na kutokana na kutojulikana sababu za mauaji hayo.
Hofu ya wafanyabiashara na wamiliki wa mabasi ya abiria mkoani Mwanza ilitolewa na Joseph Kasheku ‘Msukuma’ alipozungumza kwa niaba ya wenzake siku ya mazishi Machi 16 na kuviomba vyombo vya dola kuchunguza suala hilo ili kuwabaini wahusika na sababu za kufanya hivyo.
“Mauaji haya yameibua hofu na wasiwasi mwingi miongoni mwetu wafanyabiashara ya usafirishaji wa abiria mkoani Mwanza kwa sababu hatujui kwa nini mwenzetu katekwa na kuuawa wala hatuelewi nani atafuata miongoni mwetu,” alisema Msukuma ambaye pia ni Mbunge wa Geita Vijijini.
Josia alitoweka tangu Februari 27, siku moja baada ya kushiriki kikao cha kamati ndogo ya Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) Mkoa wa Mwanza kilichofanyika jijini Mwanza Februari 26.
Machi 9, gari lake lilikutwa likiwa limeteketezwa kwa moto ndani ya eneo la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara, siku tano kabla ya mwili wake kukutwa ndani ya maji katika Mto Ndabaka ukiwa umefungwa kwenye viroba.
Akizungumzia tukio hilo, ofisa habari wa Taboa, Mustapher Mwalongo alilitaja kuwa ni la kusikitisha na kuogofya na kuviomba vyombo vya dola kufanya uchunguzi ili kuwanasa wahusika, huku mmoja wa mawakala wa tiketi za mabasi wa Kituo Kikuu Nyegezi, Leonard Joseph akisema kifo hicho kilipokewa kwa mshtuko na wadau wa usafirishaji kutokana na mazingira yake na ukaribu wa Josia na watu waliomzunguka.
Na Johari Shani, Mwananchi
Social Plugin