Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YATOA TAMKO KUINGIA KWA UGONJWA WA DENGUE TANZANIA

WAZIRI wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amewashauri wananchi kwenda vituo vya tiba haraka mara baada ya kugundua kuwa wana dalili za ugonjwa wa dengue.


Hayo ameyasema wakati alipotoa tamko juu ya kuingia kwa ugonjwa wa dengue hapa nchini mara baada ya kufunga Mkutano wa 65 wa Jumuiya ya Mawaziri wa Afya wa Nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini ECSA jana jijini Dar es salaam.


“Kuna dalili za Ugonjwa Dengue zikiwemo homa ya ghafla, kuumwa kichwa hususan sehemu za macho, maumivu ya viungo na uchovu. Dalili hizi huanza kujitokeza kati ya siku 3 hadi 14 tangu mtu alipoambukizwa virusi vya homa ya Dengue hivyo Wizara inashauri kuwa wananchi wasiwe na hofu, bali mara tu wanapoona dalili za ugonjwa waende katika vituo vya tiba " alisema Waziri Ummy.


Aidha Waziri Ummy amesema kuwa Wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za malaria hivyo basi wananchi wanaaswa kuwa, wakipata homa wahakikishe kuwa wanapima ili kugundua kama wana vimelea vya malaria au Dengue, au sababu nyingine, ili hatua stahiki zichukuliwe.


Waziri Ummy amesema kuwa ili kujikinga na ugonjwa huo ni lazima Kuangamiza mazalio ya mbu kwa kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama au nyunyuzia dawa ya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi hayo pamoja na Kujikinga na kuumwa na mbu kwa kuvaa nguo ndefu muda wote hasa nyakati za mchana.


Aidha Waziri Ummy amesema kuwa Wizara itaendelea Kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa nchi nzima kwa kutumia mfumo uliopo wa ukusanyaji wa taarifa (IDSR), ambapo tunaendelea kupata taarifa za kila siku juu ya mwenendo wa ugonjwa huu na Kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari.


Mbali na hayo Waziri Ummy amesisitiza kuwa hakuna vikwazo vyovyote vilivyowekwa kwa ajili ya wasafiri wanaoingia na wanaotoka nchini na Wizara itaendelea kushirikiana na wadau na sekta mbalimbali katika kufuatilia na kudhibiti ugonjwa huo.


Homa ya Dengue ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vinavyoenezwa na mbu wa aina ya Aedes ambao ni weusi wenye madoa madoa meupe yenye kung’aa.

NA WAMJW-DAR ES SALAAM.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com