Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Picha : SHUWASA YATOA ELIMU YA MAJI KWA WANAWAKE SHINYANGA KUADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI


Katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani,Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Shinyanga (SHUWASA) imeendesha semina kwa wanawake wa manispaa ya Shinyanga kuwapa elimu kuhusu utoaji huduma ya maji safi na usafi wa mazingira.

Mgeni rasmi katika semina hiyo iliyofanyika leo Jumatano Machi 7,2018 katika ukumbi wa Shinyanga Vijana Centre Mjini Shinyanga alikuwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro.

Akifungua semina hiyo,Matiro aliushukuru uongozi wa SHUWASA kwa kuthamini umuhimu wa akina mama katika jamii akieleza kuwa akina mama ni muhimili mkubwa katika malezi ya familia na jamii lakini pia ndiyo walengwa wakubwa wa huduma ya maji katika maisha ya kila siku.

"Kwa kuzingatia kauli mbiu ya kitaifa ya mwaka huu inayosema 'Kuelekea uchumi wa viwanda: Tuimarishe usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake vijijini',ni dhahiri kuwa taifa limetambua nafasi ya mwanamke katika jamii,SHUWASA nawashukuru kwa kuwapa kipaumbele akinamama katika uendelezaji na usimamizi wa mipango na mikakati ya huduma ya maji safi",alisema.

"Akina mama ni nguzo muhimu sana katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za maji kwani huduma ikiwa dhaifu,waathirika wakubwa wa hali hiyo ni akina mama na watoto hivyo ni vyema wadau wote tukashirikiana kutatua changamoto zinazojitokeza",aliongeza Matiro.

Naye Mkurugenzi wa SHUWASA, Injinia Sylivester Mahole alisema SHUWASA inatambua umuhimu wa akina mama katika huduma zake za kusambaza maji safi katika manispaa ya Shinyanga na inaunga mkono kauli mbiu ya kisekta ya “Kumtua Mwanamke ndoo kichwani”.

“Katika kuadhimisha siku wanawake duniani ambayo huadhimishwa kila tarehe 8 Machi,SHUWASA imeona umuhimu wa kukutana na wadau wetu wakubwa,sote tunafahamu kuwa akina mama ndiyo watumiaji wakubwa wa maji katika jamii”,alisema Injinia Mahole.

"Tumewaiteni hapa ili kuwapa elimu kuhusu huduma zetu kwa lengo la kuimarisha uwazi katika utekelezaji wa majukumu ya SHUWASA kwa kutambua umuhimu wa akina mama katika kuboresha huduma ya maji safi na usafi wa mazingira katika manispaa ya Shinyanga ",aliongeza Mahole.

Wakizungumza katika semina hiyo, akina mama waliipongeza SHUWASA kwa kuendelea kuboresha huduma zake ikiwemo kutuma ujumbe mfupi wa maneno (SMS) kwa njia ya simu pindi ankara za maji zinapotoka lakini pia kuwakumbusha wateja kulipa ankara zao wanapojisahau. 

"Hivi sasa hatusumbuki wala kupoteza muda kwenda kulipia bill 'ankara' dirishani,sasa tunalipa kwa njia ya simu au benki,tunaomba SHUWASA ifikishe huduma kwenye maeneo ambayo hajafikiwa ili kuwatua ndoo kichwani wanawake ambao hawajafikiwa na huduma ya maji",alisema Happiness Mwaja na Elizabeth Ndagwa.

Kwa upande wake Marietha Mwakisu aliishauri SHUWASA kuweka utaratibu wa kufuatilia mitandao ya maji kwenye barabara kwani mabomba yamekuwa yakipasuka na kusababisha upotevu maji.

ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akifungua semina ya wanawake wa Manispaa ya Shinyanga iliyoandaliwa na SHUWASA kama moja ya matukio ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza katika semina hiyo.Wa kwanza kushoto ni Makamu mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi SHUWASA, Joyce Egina.Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa SHUWASA, Injinia Sylivester Mahole akifuatiwa na mwenyekiti wa semina hiyo, Ziphora Pangani (Mkuu wa wilaya mstaafu).
Akina mama wa Manispaa ya Shinyanga wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na wanawake wa manispaa ya Shinyanga.
Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Shinyanga (SHUWASA), Injinia Sylivester Mahole akiwasisitiza akina mama kuendelea kushirikiana na SHUWASA katika kutatua changamoto zinazojitokeza katika utoaji huduma za maji safi na usafi wa mazingira.
Akina mama wakiwa katika semina hiyo.
Makamu mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi SHUWASA, Joyce Egina akizungumza wakati wa semina hiyo.
Wafanyakazi wa SHUWASA wakiwa ukumbini: Wa kwanza kushoto ni Afisa Uhusiano wa SHUWASA,Nsianeli Gelard ,katikati ni Afisa TEHAMA SHUWASA,Amosi Stephen akifuatiwa na Meneja Utawala na Rasilimali Watu SHUWASA, Flaviana Kifizi.
Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Shinyanga (SHUWASA), Injinia Sylivester Mahole akielezea kuhusu majukumu ya SHUWASA pamoja na kuanzishwa kwa siku ya wanawake duniani ambayo huadhimishwa kila tarehe 8 mwezi Machi.
Injinia Sylivester Mahole alisema SHUWASA inatambua mchango mkubwa wa wanawake katika jamii ndiyo maana wameamua kutoa elimu ya huduma za maji kwani wanawake ndiyo wadau wakubwa wa SHUWASA.
Afisa Uhusiano wa SHUWASA,Nsianeli Gelard akitoa mada kuhusu mkataba wa huduma kwa wateja. Aliwataka wateja kutoruhusu vitendo vya rushwa katika huduma za maji na kuwataka wateja kutunza mita za maji na kuhakikisha wanalipa ankara za maji kwa wakati.
Afisa Uhusiano wa SHUWASA,Nsianeli Gelard akiendelea kutoka mada kuhusu mkataba wa huduma kwa wateja. Alisema SHUWASA inaendelea kutoa elimu ya maji kwa makundi mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa shule za sekondari.
Afisa TEHAMA wa SHUWASA, Amosi Stephen akielezea jinsi walivyoboresha huduma za ulipaji wa ankara za maji ambapo hivi wateja sasa wanafurahia huduma na kutumia simu na benki kulipa ankara za maji.
Mwenyekiti wa semina hiyo, Ziphora Pangani (Mkuu wa wilaya mstaafu) akiongoza kipindi cha majadiliano wakati wa semina.
Esha Stima akichangia hoja wakati wa semina hiyo.
Mwinjilisti Esther Emmanuel akichangia hoja ukumbini.
Katibu wa TCCIA mkoa wa Shinyanga Marcelina Saulo akichangia hoja wakati wa semina hiyo.
Marietha Mwakisu akizungumza ukumbini.
Mkurugenzi wa Easyflex Production Studio,Happiness Kihama akichangia hoja wakati wa semina hiyo.
Bora Yusuph akizungumza wakati wa semina hiyo.
Mwenyekiti wa mtaa wa Magadula kata ya Ngokolo,Diana Ezekiel
Joyce Masunga (mbunge mstaafu) akichangia hoja wakati wa semina hiyo.
Baadhi ya wafanyakazi wa SHUWASA wakiwa katika semina hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro na akina mama wakicheza muziki/wimbo wa Wanawake na Maendeleo.
Akina mama na mkurugenzi wa SHUWASA Injinia Sylivester Mahole wakiendelea kucheza muziki.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com