SNURA ALIA CHURA WAKE KUFUNGIWA MARA MBILI MBILI


Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Snura Mushi, amesema hadi sasa haelewi ni kwanini nyimbo zake mbili zimefungiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).


Akizungumza Machi 3, Snura amesema kufungiwa kwa nyimbo zake mbili ya ‘Chura’ na ‘Nimevurugwa’ kumemchanganya na wala haelewi hadi sasa nini sababu ya kufikiwa kwa hatua hiyo na mamlaka hiyo ya Serikali.

Akitolea mfano wa wimbo wa ‘chura’ Snura amesema video yake ilipofungiwa alitakiwa kuirekebisha na alifanya hivyo na kisha ikahaririwa na vyombo vyote ikiwamo Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na TCRA wenyewe na kumruhusu kuionyesha.

“Lakini juzi nashangaa kati ya nyimbo 15 zilizofungiwa yangu hiyo ya chura nayo ilikuwa mojawapo hadi najiuliza kumetokea nini hasa hadi wanipe adhabu hiyo kubwa kwangu,” amesema Snura.

Wakati kwa wimbo wake wa ‘Nimevurugwa’ amesema ana uhakika hakuna tusi lolote ndani ya wimbo huo na kueleza hata video yake haoni kama ina shida.

Pia msanii huyu ameeleza pamoja na yote hayo hajapewa barua hadi sasa kama ilivyo taratibu msanii unapotaka kufungiwa nyimbo yako na wala Basata haijamuita kumweleza tatizo lake ni nini hasa.

Kutokana na hatua hiyo, MCL Digital, pia iliweza kuongea na Mkurugenzi wa TCRA, Mhandisi James Kilaba, ili kujua ni vigezo gani walivyotumia katika kuzifungia nyimbo walizozitaja ukizingatia nyingine zilishafungiwa kipindi cha nyuma na wasanii kulipishwa faini.

Katika majibu yake, Mhandisi Kilaba, amesema swali hilo waulizwe Basata kwa kuwa wao ndio waliwapelekea malalamiko kuhusu nyimbo hizo na kwa kuwa moja ya kazi yao ni kusimamia redio na televisheni ndio wakaamua kuchukua hatua hiyo ya kuviandikia barua vyombo hivyo kuacha kuzionyesha na kuzicheza.

Wakati Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza, amesema walichukua hatua ya kupeleka malalamiko yao TCRA, baada ya kuona pamoja na kuzifungia nyimbo hizo lakini bado baadhi ya vituo vya redio na televisheni ziliendelea kuzicheza na wao hawana mamlaka ya kuvichukulia hatua vyombo hivyo zaidi ya kuishia kwa wasanii.

Februari 28 TCRA iliandika barua kwa vituo vya redio na televisheni ikiviagiza visitishe kuonyesha nyimbo 15 za wasanii kadhaa kutokana na kuwa na maudhui ambayo yanaenda kinyume na maadili na kanuni za Huduma za Utangazaji (Maudhui) 2005.

Nyimbo hizo na jina la msanii aliyeimba kwenye mabano ni Hallelujah na Wakawaka (Diamond), Kibamia (Roma Mkatoliki), Pale Kati patamu, Maku (Makuzi) na Mikono Juu (Ney wa Mitego), Hainaga Ushemeji (Manifongo), I am Sorry JK (Nikki Mbishi).

Nyingine ni Chura na Nimevurugwa (Snura), Tema mate tumchape (Madee), Uzuri wako (Jux), Nampa papa (Gigy Money), Nampaga (Baranaba) na Bongo Bahati mbaya (Young D).
Chanzo- Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post