Klabu ya Stand United imefanikiwa kutinga hatua nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho, baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Njombe Mji FC jioni ya leo kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga.
Bao pekee lililowapeleka mbele wenyeji limefungwa na Abdul Swamad dakika ya 12 akimalizia krosi ya Vitalis Mayanga ambaye naye alipokea pasi ya beki Eric Mulilo aliyepanda vizuri upande wa kulia kusaidia mashambulizi.
Licha ya ushindi huo lakini Stand United ilimaliza dakika 90 ikiwa na wachezaji 10 uwanjani baada ya Nahodha wake, Erick Mulilo kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 80 kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.
Stand sasa itasubiri kujua inakutana na nani katika hatua ya nusu fainali ambapo timu kama Yanga, Singida United, Azam FC na Mtibwa Sugar zinacheza mechi zake za robo fainali kuanzia kesho hadi April 1.