Shirika la Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema uamuzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) kusimamisha masomo mwanafunzi wake, Abdul Nondo kabla ya kumalizika kwa kesi inayomkabili mahakamani, ni sawa na kumhukumu kabla ya kesi hiyo kumalizika.
Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Willima Anangisye amemsimamisha masomo Nondo baada ya kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kubainisha kuwa kesi hiyo ikimalizika, ataendelea na masomo.
Wakati THRDC na LHRC wakieleza hayo, Nondo ameahidi kuelekeza masuala mbalimbali katika waraka wake anaotarajia kuutoa siku za hivi karibuni baada ya afya yake kuimarika.
Wakizungumza leo Machi 27, 2018 mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa amesema ndiyo maana Nondo alipewa dhamana mahakamani ikiwa ni ishara ya kumpa nafasi ya kuendelea na masuala mengine, yakiwamo masomo.
Amesema uamuzi wa UDSM unakwenda kinyume na haki za binadamu na Katiba ya nchi.
Amesema kuna haja ya kwenda mahakamani kuhoji jambo hilo kwa maelezo kuwa wapo watumishi wanaofikishwa mahakamani, lakini bado wanaendelea na kazi zao.
" Nondo hata kesi yake ukiangalia aliripoti kama mlalamikaji lakini kilichotokea ndiyo hicho sasa kabla ya ukweli haujajulikana chuo nao wanatoa uamuzi huo kwa kweli hawajamtendea haki mwanafunzi huyu,"amesema.
Mkurugenzi wa LHRC, Hellen Kijo-Bisimba amesema ilipaswa kuangaliwa mazingira ya kesi ya Nondo kwa maelezo kuwa mara ya kwanza ilielezwa ametekwa, kisha mashtaka kubadilishwa kuwa amejiteka.
“Walichokifanya kwa Nondo ni uonevu ukizingatia mazingira magumu aliyonayo sasa na baada ya kukaa muda mrefu mahabusu bila kuonana na mtu yeyote na wala hakuna aliyejua amefanywa nini huko mpaka leo,” amesema.
Amesema pamoja na kwamba kanuni hizo ni za UDSM, kisheria hazifai kutumika kwa kuwa zinaenda kinyume na haki za binadamu.
Nondo amesema hadi sasa hajapata barua hiyo ya kusimamishwa kuendelea na masomo, zaidi ya kuonyeshwa na wanafunzi wenzake.
Amesema kwa sasa hana cha kuzungumza hadi atakapopatiwa rasmi barua hiyo ili kujua sababu za kusimamishwa kwake.
Kuhusu tetesi za kuwahi kupewa barua za onyo mara mbili na uongozi wa UDSM, amesema kwa sasa hayupo tayari kulizunguzia suala hilo.
Ameahidi kuelekeza masuala mbalimbali katika waraka wake anaotarajia kuutoa siku za hivi karibuni baada ya afya yake kuimarika.
Na Nasra Abdallah, Mwananchi
Social Plugin