Taarifa kwa vyombo vya habari | 29 Machi 2018
Zaidi ya nusu ya watanzania hawajisikii huru kumkosoa Rais, Makamu wa Rais na Waziri mkuu
Hata hivyo wananchi 8 kati ya 10 wanasema wanapaswa kuwa huru kumkosoa Rais na serikali
29 Machi 2018, Dar es Salaam: Idadi kubwa ya wananchi hawajisikii huru kumkosoa Rais (60%), Makamu wa Rais (54%) na Waziri Mkuu (51%). Karibu nusu ya wananchi pia hawajisikii huru kuwakosoa mawaziri (47%), Wakuu wa Mikoa (46%) na Wakuu wa Wilaya (43%). Hata hivyo, idadi kubwa ya wananchi (87%) wanasema wanapaswa kuwa huru kuikosoa serikali na Rais kwa kufanya maamuzi mabaya na kutosikiliza ushauri (80%). Wanaamini kupitia ukosoaji wanaweza kuisaidia serikali kutofanya makosa (81%) na si kuwashushia hadhi watendaji wa umma au kuhatarisha umoja (19%). Vilevile wananchi hawaungi mkono matumizi ya lugha ya matusi ambapo asilimia 71 ya watanzania hawataki wananchi waruhusiwe kuwaita wafuasi wa chama chochote cha siasa “wapumbavu au malofa”.
Matokeo haya yametolewa na Twaweza katika muhtasari wake uitwao Siyo kwa kiasi hicho? Maoni ya wananchi kuhusu taarifa na mijadala. Takwimu za muhtasari huu zinatokana na utafiti wa Sauti za Wananchi ambao huratibiwa na taasisi ya Twaweza.Sauti za Wananchi ni utafiti wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi. Una uwakilishi wa Tanzania Bara pekee, Zanzibar haihusiki kwenye utafiti huu. Kwa maelezo zaidi kuhusu mbinu za utafiti huu tembelea www.twaweza.org/sauti. Takwimu za muhtasari huu zilikusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,519 kutoka awamu ya 25 ya kundi la pili la Sauti za Wananchi, na zilikusanywa kati ya Novemba 7 na Novemba 27 mwaka 2017.
Wananchi wengi wana imani kubwa na taarifa zinazotolewa na Rais (70%) na Waziri Mkuu (64%). Idadi ndogo zaidi wanamwamini mwenyekiti wao wa kijiji (30%), wabunge (wa chama tawala 26%, wa upinzani 12%), na viongozi wa serikali kwa ujumla (22%).
Wananchi pia wanaendelea kuunga mkono kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa taarifa: wananchi 7 kati ya 10 wanasema taarifa zinazomilikiwa na mamlaka za umma ni mali ya umma (70%, juu zaidi kutoka 60% mwaka 2015); na wananchi 9 kati ya 10 wanasema wananchi wa kawaida wapate taarifa zinazomilikiwa na mamlaka za umma (86%, juu zaidi kutoka 77% mwaka 2015) na kwamba kwa kuwapa wananchi uwezo wa kupata taarifa kunaweza kupunguza rushwa (86%, juu zaidi kutoka 80% mwaka 2015).
Pamoja na kuunga mkono kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa taarifa, wananchi 9 kati ya 10 hawajawahi kuomba taarifa kutoka katika ofisi za serikali (95%), mamlaka za maji (93%), au vituo vya afya (93%). Wananchi wameendelea kutumia vyanzo vile vile vya habari bila kuwa na mabadiliko makubwa isipokuwa kwa upande wa runinga: mwaka 2013 runinga ilikuwa ni chanzo kikuu cha taarifa kwa 7% ya wananchi, mwaka 2017 ni asilimia 23 ya wananchi. Hata hivyo, imani kwa aina mbalimbali za vyanzo vya habari inashuka – radio kutoka 80% mwaka 2016 hadi 64% mwaka 2017, runinga kutoka 73% mwaka 2016 hadi 69% mwaka 2017 na maneno ya kuambiwa kutoka 27% mwaka 2016 hadi 13% mwaka 2017.
Pamoja na kushuka kwa imani na vyombo vya habari, wananchi bado wanaunga mkono uhuru wa vyombo vya habari: wananchi wanasema gazeti lililochapisha taarifa za uongo ama zisizo sahihi liombe radhi na kuchapisha marekebisho (62%) badala ya gazeti hilo kufungiwa ama kutozwa faini (38%). Idadi kubwa ya wananchi pia wanasema kuwa serikali ipate ridhaa ya mahakama katika kufanya maamuzi yoyote ya kuliadhibu gazeti kwa kutoa taarifa zenye maudhui yasiofaa (54%).
Japokuwa wananchi wana mtazamo thabiti kuhusu upatikanaji wa taarifa na uhuru wa kuzungumza, ni wananchi wachache sana wanaofahamu sheria zinazohusiana na masuala ya habari. Sheria inayofahamika zaidi katika suala hili ni Sheria ya Makosa ya Mtandao (2015), ambayo inafahamika na asilimia 10 ya wananchi huku asilimia 4 pekee ya wananchi wakifahamu Sheria ya Huduma za Habari (2016). Wananchi wengi pia hawajaunganishwa kwenye mifumo ya uraia ambapo ni mwananchi 1 kati ya 4 au pungufu mwenye cheti cha kuzaliwa (25%), kitambulisho cha uraia (21%), leseni ya udereva (9%) na hati ya kusafiria (5%). Hata hivyo, karibu wananchi wote (98%) wana vitambulisho vya mpiga kura
Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, anasema: “wananchi wanaunga mkono kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa taarifa na uhuru wa kujieleza. Lakini ukweli wa mambo ni kwamba, wananchi hawaombi taarifa hizo, wana imani duni na vyanzo vyote vya taarifa ukiweka kando kauli zinazotolewa na Rais na Waziri Mkuu, na hawajioni kama wanaweza kuwakosoa viongozi wakuu wa serikali.”
“Kutokana na kwamba hivi karibuni serikali imepitisha kanuni za Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa
tuna imani kuwa itakidhi kiu ya wananchi ya kupata taarifa kutoka serikalini. Tunaishauri serikali kuweka wazi taarifa ili kuyafikia matarajio ya wananchi. Cha kusikitisha, wananchi wanakamatwa na serikari kwa kujieleza kupitia mitandao ya kijamii. Ni vyema serikali ikatambua thamani ya mijadala huru ya umma na ukosoaji wenye lengo la kujenga katika mapambano dhidi ya rushwa na katika harakati za kuelekea kuwa nchi ya uchumi wa kati.”
---- Tamati ----
Kwa taarifa zaidi wasiliana na:
Risha Chande, Mshauri Mwandamizi wa Mawasiliano, Twaweza e: rchande@twaweza.org | t: (+255) (0) 656 657 559
Maelezo kwa Wahariri
- Muhtasari huu na takwimu zilizomo vinaweza kupatikana kwenyewww.twaweza.org
- Twaweza inafanya kazi kuwezesha watoto kujifunza, wananchi kuwa na utayari wa kuleta mabadiliko na serikali kuwa wazi zaidi na sikivu katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda. Tuna programu, wafanyakazi na ofisi katika nchi zote tatu, na utaratibu unaoheshimika kimataifa wa kujifunza, ufuatiliaji na tathmini. Programu zetu muhimu ni pamoja na Uwezo, tathmini kubwa ya kila mwaka ya wananchi barani Afrika inayopima viwango vya watoto vya kujifunza kwenye maelfu ya kaya, na Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika kwa njia ya simu ya mkononi. Pia tunashiriki kwenye masuala ya umma na sera, kupitia ubia wetu na vyombo vya habari, juhudi za kimataifa zinazoshughulikia masuala ya uongozi kama vile mpango wa Ushirikiano na Serikali wazi (OGP).
- Unaweza kufuatilia kazi za Twaweza
- Tovuti: www.twaweza.org Facebook: Twaweza Tanzania Twita @Twaweza_NiSisi
Social Plugin