Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu Boniface Butondo akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya Kishapu mkoani Shinyanga, ambapo alisema wanatambua jitihada kubwa zinazofanywa na mtandao wa jinsia Tanzania TGNP kupitia vituo vyake vya taarifa na maarifa katika kuibua changamoto mbalimbali za kijamii,huku akiahidi kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyowasilishwa kwenye kikao hicho na wanamtandao kwa niaba ya wanajamii juu ya bajeti ya halmashauri ya mwaka 2018/2019.
Wanaharakati wa mtandao wa jinsia Tanzania TGNP Kishapu ,katibu wa mtandao Peter Nestory akisoma taarifa ya Mtandao.
Madiwani wa halmashauri ya Kishapu wakiwa kwenye kikao cha baraza la madiwani wakipitia taarifa mbalim bali kwenye makabrasha
Wanaharakati kutoka vituo vya taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu wakifuatilia kikao cha baraza la madiwani.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Kishapu Boniface Butondo akiendelea na kikao.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Kishapu Stephen Magoiga akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani.
Madiwani wakiendelea na kikao.
***
Halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imeshauriwa kuanzisha kamati za ulinzi wa mtoto ili kupambana na ukatili wa kijinsia kuanzia ngazi ya jamii na kuandaa mpango na bajeti, kukabiliana na changamoto hiyo na kuhakikisha shule zinakuwa na vyumba maalumu vya watoto wa kike wakati wa hedhi.
Hayo yalielezwa hivi karibuni na katibu wa mtandao wa vituo vya taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu vinavyosimamiwa na TGNP Mtandao Peter Nestory, wakati akiwasilisha mapendekezo ya wanajamii katika kikao cha baraza la madiwani , kupitia hoja binafsi waliyoiandaa ikilenga bajeti ya halmashauri hiyo ya 2018/2019 ambayo haikutenga kifungu kununua taulo ama pedi kwa wanafunzi wa kike.
Katika mapendekezo hayo wameishauri halmashauri kupitia bajeti ndogo kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba maalumu kwa shule za msingi na sekondari na kununua pedi kwa watoto wa kike,huku wakipongeza bajeti ya mwaka 2017/2018 ilizingatia mlengo wa kijinsia na kuchangia halmashauri kupatiwa tuzo.
“Kupitia mapendekezo yetu tunashauri shilingi milioni 40 zilizotengwa kwenye bajeti ya mwaka 2018/2019 kwa ajili ya kuwezesha makundi ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu haiwezi kukidhi malengo kwani bajeti ya mwaka uliopita walitenga shilingi milioni 82 lakini hazikutosha ni vema ikaongezwa na kufikia shilingi milioni 100 au ipelekwe eneo moja”alisema katibu.
Pia waliishauri halmashauri na serikali kupitia wizara ya afya,maendeleo ya jamii,jinsia wazee na watoto kuchukuwa hatua za makusudi ili kuweza kukamilisha ujenzi zahanati na vituo vya afya pamoja na kuboresha upatikanaji wa vifaa tiba na madawa hatua itakayosaidia kuepusha vifo vya mama na mtoto chini ya miaka mitano.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri hiyo Boniface Butondo alisema wanatambua jitihada kubwa zinazofanywa na mtandao wa jinsia Tanzania TGNP kupitia vituo vyake vya taarifa na maarifa,huku akiahidi kuyafanyia kazi mapendekezo hayo ili kuleta tija zaidi katika halmashauri hiyo na wananchi kwa ujumla.
Alisema mtandao huo uliiwezesha halmashauri hiyo kupata tuzo ambayo ilikabidhiwa na makamu wa rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kutokana na kupitisha bajeti ya mwaka 2016/2017 iliyozingatia mlengo wa kijinsia ambayo iliwawezesha watoto wa kike kupata pedi/taulo na kuahidi kuzingatia ushauri huo.
Naye mkurugenzi wa halmashauri hiyo Stephen Magoiga alisema hoja na mapendekezo ya wanajamii yaliyowasilishwa na katibu wa mtandao huo wilaya ya Kishapu,watayajibu kwa maandishi ikiwa ni pamoja na kutolea ufafanuzi wa mikakati iliyopo na hatua iliyochukuliwa.
Habari hii imeandaliwa na mwandishi wa Malunde1 Blog.