WANAFUNZI 400 WAVUNJA NYUMBA YA MWALIMU...SHULE YAFUNGWA

Serikali imeifunga Shule ya Sekondari ya Lyamungo iliyoko Hai mkoani Kilimanjaro, baada ya wanafunzi wake kuzusha vurugu kubwa huku wakivamia na kuivunja ofisi ya Makamu Mkuu wa shule hiyo.


Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Hai, Onesmo Buswelu, alithibitisha jana kuifunga sekondari hiyo ya kitaifa kuanzia Machi Mosi hadi Machi 17, mwaka huu.


Shule hiyo ya kitaifa hupokea wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita kutoka mikoa mbalimbali nchini.


"Ni kweli nimeifunga hiyo shule kwa zaidi ya wiki mbili kutokana na sababu za kiusalama. kulikuwa na uchaguzi wa serikali ya wanafunzi na wakati unafanyika mwanafunzi mmoja aliandika matusi makubwa akiwatukana walimu.


"Baada ya kufanyika uchunguzi aligundulika huyo mwanafunzi na hapo ndiko walipoandaa vurugu hizo na kujielekeza kuharibu mali na kusababisha hasara ambayo bado haijafahamika," alisema Buswelu.


Kwa mujibu wa Buswelu, vurugu hizo ziliibuka baada ya mwanafunzi huyo (jina limehifadhiwa) kupewa barua ya kufukuzwa shule kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu.


Buswelu ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Siha ameagiza Bodi ya shule hiyo kukutana kesho (leo) kufanya tathmini ya hali ya uharibifu na madhara yaliyojitokeza na kuiarifu serikali.


Mpaka sasa, hakuna mwanafunzi anayeshikiliwa kwa kufanya vurugu na kusababisha hasara ya mali na rasilimali za serikali.


Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Hamisi Issah, alisema wanafunzi hao walifanya tukio hilo saa 4:30 usiku juzi.


"Hao wanafunzi wameharibu ofisi ya mwalimu huyo ambaye pia ni mwalimu wa nidhamu kwa kuvunja paa la juu, milango, madirisha na samani za ndani," alisema Kamanda Issah.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post